Friday, March 08, 2013

TUME YA UCHUNGUZI WA KUSHUKA UFAULU KIDATO CHA NNE 2012 YAWAOMBA WATANZANIA KUTOA USHIRIKIANO.

Mkiti wa Tume 1 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 Prof. Sifuni Mchome (katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka wadau mbalimbali. Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene (kushoto) na Bi.Tunu Temu mjumbe wa Sekretarieti ya Tume hiyo.
…………………………………………………………………              
Na. Aron Msigwa -MAELEZO, Dar es salaam.
 Tume ya Taifa iliyoundwa na Mh. Waziri mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 imewaomba watanzania kuipa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili iweze kukamilisha majukumu iliyopewa kwa muda na ufanisi mkubwa.
 Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof.Sifuni Mchome ameeleza kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya kuzinduliwa na Waziri mkuu tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua kuwa jukumu lililopo sasa ni kuanza kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa watanzania ili kubaini sababu za matokeo mabaya ya mtihani huo.
 Amesema kuwa tume hiyo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu nchini huku mapendekezo hayo  yakizingatia kipindi cha muda mfupi , kati na kipindi cha muda mrefu.
 Prof. Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia hadidu mbalimbali  za rejea zikiwemo kubainisha sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012, sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari katika halmashauri zake. 
  Rejea nyingine ni pamoja na pamoja na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali ya matokeo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua mara moja kwa wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao kwa kupata daraja sifuri.
 Amefafanua kuwa tume katika kutekeleza majukumu yake itapitia mitaala na mihutasari ya Elimu ya Msingi na Sekondari, kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji na ufunzaji, kuangalia mfumo wa upimaji na tathmini ya mitihani pia usimamizi na uendeshaji.
 Pia pamoja na mambo mengine tume itatathmini mchango wa jamii na wazazi/ walezi katika maendeleo ya wanafunzi, hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana, upungufu wa majengo ya shule,madarasa, maabara na maktaba.
Vilelevile tume hiyo itafuatilia mwamko wa wazazi katika kufuatilia mkazo wa eliimu kwa watoto na suala la mmomonyoko wa maadili unaotokana na ukuaji wa utandawazi hususan teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kutathmini athari ya mfumo wa ufundishaji wa  mikondo miwili iliyopo katika shule za Zanzibar.
 Aidha mwenyekiti wa Tume hiyo amebainisha kuwa tume itaanza rasmi kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kupata maoni kuanzia tarehe 11 mwezi huu kwa kuanza na mkoa wa Dar es salaam, Zanzbar na maeneo mengine nchini kwa kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali za Wizara, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Shule, Taasisi mbalimbali za kijamii na wananchi kwa ujumla na pia kuwasilisha maoni kwenye tume kupitia Mwenyekiti wa Tume, Tume K4-2012, S.L.P 5909 Dar es salaam au kupitia simu 0737206038, Barua pepe: maoni@tumek4.go.tz au kwa kutembelea Tovuti ya tume ya www.tumek4.go.tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...