Rais Xi Jinping wa China ameahidi
kuendelea kuipiga jeki Afrika ili kukabiliana na changamoto za
kimaendeleo, huku akisema kuwa suala la utoaji misaada yenye masharti
magumu siyo ajenda ya Serikali yake. Jinping akitumia jukwaa la Tanzania
kutambulisha sera yake kwa nchi za Afrika alisema kwamba bara hilo
limepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba nchi yake itaimarisha
uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Alisisitiza kwamba ushirikiano wenye tija ni ule
unaozingatia “majadiliano na maridhiano” na kwamba Serikali yake
imetenga kiasi cha Dola za Marekani 20 bilioni kufadhilia miradi
mbalimbali ya maendeleo Afrika.
“China haitakuwa tayari kutoa masharti kwa
taifa lolote… Tunataka kutoa fursa zinazofanana,” alisema Rais, ambaye
alishika rasmi wadhifa huo Machi 14, mwaka huu. Alisema China
haitaingilia masuala ya ndani ya nchi, huku akisisitiza kwamba shabaha
ya nchi yake ni kuendelea kupalilia ushirikiano mwema uliodumu kwa
miongo kadhaa na siyo kujihusisha na migogoro.
Baadhi
ya wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, kauli ya kiongozi hiyo ni kama
ujumbe wa onyo kwa baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zinalalamikiwa
kuendesha sera zinazominya ustawi wa Afrika.
Mhadhiri katika
Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR), Dk Ahmed Mtengwa
alisema: “Ni hotuba inayofungua njia kwa Afrika..., amezungumzia
ushirikiano unaolingana yaani `win win situation’ (kila upande
ufaidike), hivyo kwangu ninayaona matumaini.”Rais Jinping,
aliyekuwa katika ziara ya siku mbili nchini na juzi usiku alisaini
mikataba 17 inayohusu sekta za kilimo, afya na miundombinu.
Mkataba
wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ni kati ya miradi mikubwa
iliyomo kwenye makubaliano hayo na ujenzi wake utafanywa na Kampuni ya
Merchants Holding ya China na utakwenda sanjari na ujenzi wa barabara
inayounganisha bandari hiyo.
Pia katika
bandari hiyo itaunganishwa na Reli ya Kati na na ile ya Mamlaka ya Reli
ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili kurahisisha usafiri wa mizigo ndani
na nje ya nchi. Mikataba mingine itahusiana na uboreshaji wa sekta ya
viwanda, kilimo hasa kile cha tumbaku ikiwamo kuwatafutia soko wakulima
kutoka Mikoa ya Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko
la China pamoja na kulipatia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zana
za kufanyia kazi.
Rais huyo, ambaye Tanzania ndiyo nchi
ya kwanza barani Afrika kuitembelea, alizindua na kukabidhi rasmi Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichoko jijini
Dar es Salaam ambalo ni jengo la ghorofa tatu na lenye kumbi nne za
mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 1,800 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa kituo
hicho uligharimu Dola za Marekani 29.7 milioni zilizotolewa na Serikali
ya China kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais huyo
alisifu ushirikiano wa muda mrefu baina ya taifa lake na Tanzania na
kusisitiza kuwa nchi hizo zitaendelea kusaidiana kama sehemu ya kuenzi
misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Mwalimu Julius
Nyerere na Mao Tse Tung.
Rais
Jinping aliondoka jana jioni kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa
tano wa Wakuu wa Nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi ikiwamo Brazil, Urusi,
India, China na Afrika ya Kusini (BRICS).
Chanzo -
Mwananchi
No comments:
Post a Comment