Nairobi.
Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchini Kenya imeagiza kuchunguzwa kwa
fomu 34 za matokeo ya uchaguzi wa rais kutoka katika vituo vyote
34,400, vilivyotumika kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo
uliofanyika Machi 4, mwaka huu.
Kadhalika mahakama hiyo jana iliagiza
kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo vya kupigia kura 22 kati
ya elfu 33 vilivyolalamikiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa
Cord, Raila Odinga.
Katika malalamiko yake yaliyowasilishwa
katika mahakama hiyo kupinga Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais
katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 4, Odinga alidai kuwa vituo hivyo
22 kura zilizopigwa zinazidi idadi ya wapigakura walioandikishwa.
Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya majaji
wenzake watano, Jaji Smokin Wanjala alisema kwamba uhesabuji kura wa
vituo hivyo utafanyika leo kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa lengo la kubaini
ukweli kuhusu madai hayo.
“Matokeo ya kura zitakazohesabiwa katika
vituo hivyo 22 yawasilishwe katika mahakama hii Jumatano, saa 10.00
jioni,” alisema Jaji Wanjala.
Kikao hicho, ambacho Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mohamed Othman Chande amealikwa kama mwangalizi, ni cha awali
kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi keshokutwa (Alhamisi) na
kuendelea kwa mfululizo hadi kufikia uamuzi ikiwa madhumuni yake.
Lengo ni kupitia madai yaliyowasilishwa
mahakamani hapo na pande zote zinazohusika na kuamua mwenendo wa kesi
utakavyofanyika.
Ukiachilia mbali kesi iliyofunguliwa na
Odinga kupinga Kenyatta kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa tano tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa Kenya, kuna kesi nyingine
ambayo imefunguliwa na muungano wa mashirika yasio ya kiserikali, `The
African Centre for Open Governance’ (Africog).
Katika kesi hiyo inayorushwa moja kwa
moja na vituo kadhaa vya televisheni nchini Kenya, Africog inahoji
uhalali wa uchaguzi huo.
“Kesi yetu haihusiani na nani ameshinda
au kushindwa bali jinsi umma ulivyoshindwa, tumepoteza ahadi ya uchaguzi
uliowazi,” alisema Gladwell Otieno, Mkurugenzi Mtendaji wa Africog.
Kesi ya tatu ambayo imefunguliwa na
wajumbe wa timu ya kampeni ya Kenyatta, mwanaharakati katika mitandao ya
kijamii Dennis Itumbi na Moses Kuria wanaopinga uamuzi wa Tume Huru ya
uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya kujumuisha kura zilizoharibika wakati wa
kujumlisha kura za wagombea urais.
Katika uamuzi wake, mahakama iliamua
kwamba kesi zote tatu zitaunganishwa kuwa moja, huku ile iliyowasilishwa
na Odinga ikiwa ndiyo kinara wa kesi zote.
Pia mahakama iliamuru Muungano wa Vyama
vya Siasa wa Cord na Jubilee kuteua mawakala 10 kila mmoja ambao
watakula kiapo mahakamani hapo kabla ya kuanza kuhesabu upya kura hizo.
Katika uamuzi wake jana jioni, mahakama
hiyo ilikubali ombi la Mwanasheria Mkuu wa Kenya, kushiriki katika kesi
hiyo kama rafiki wa mahakama na siyo mdaiwa kama ilivyokuwa awali.
Wakili wa Cord, George Oraro alikubali uamuzi huo licha ya kuupinga
awali.
No comments:
Post a Comment