WAKATI
wanachama takribani 700 wanatarajia kufanya mkutano wa dharura leo
Mnazi Mmoja, uongozi wa klabu hiyo umepiga stop kumkutano huo kwa madai
kuwa wanachama hao hawana haki ya kuitisha mkutano wakati tayari
uongozi ulishatoa tamko la kufanya mkutano huo wa dharura wakati wowote
kuanzia sasa.
Uongozi huo wa Simba kupitia kwa ofisa habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga ulisema kuwa mkutano utakaofanyika leo ni batili kwa kuwa hauna baraka za uongozi na kuwataka wanachama wa Simba kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho mwenyekiti wao Ismail Aden Rage akiwa India kwenye matibabu na anatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa wiki ijao.
Kauli hiyo ya uongozi imekuja ikiwa leo wanachama hao wakitarajia kufanya mkutano wao kwa mujibu wa katiba yao ibara ya 22 ambayo inatamka wazi wanachama wasiopungua 500 wana haki ya kuandaa mkutnao mkuu kama mwenyekiti hayupo tayari kuitisha mkutano ndani ya siku 30.
Hata hivyo jana Kamwaga alisema "Mwezi uliopita mwenyekiti alitangaza kuitisha mkutano wa dharura siku yoyote ajenda ingekuwa moja tu kujadili mwenendo wa klabu bahati mbaya alishikwa maradhi ikabidi aende India kutibiwa, kuna uwezekano mkubwa akarejea wiki ijayo.
"Uongozi umeridhia kufanyika kwa Mkutano wa wanachama. Kimsingi, kama uongozi umeridhia, hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano mkuu mwingine, hao wanaoitisha mkutano wana nguvu gani ya kisheria kufanya hivyo? Walichaguliwa na nani kuwakilisha wanachama? Lini na wapi?" alihoji Kamwaga.
"Uongozi unaweza kuitisha mkutano kwa vile wenyewe ndiyo wenye leja ya wanachama, Klabu ina database yake ya kompyuta inayotambua wanachama walio hai na wasio hai, hakuna mtu mwingine yeyote, aliye nje ya uongozi huu anayefahamu wanachama walio hai na wasio hai hao wanachama wanaoitana kufanya mkutano, wamehakikiwa na nani kubaini uhalali wao huo?"
Alisema wanachama wanaolazimisha kufanyika kwa mkutano wana ajenda binafsi na si za maslahi ya klabu, Kama kweli wangekuwa na nia njema na klabu wangesubiri mkutano ambao utaitishwa punde na kwamba mkutano huo wa leo una lengo la kuleta vurugu na mifarakano ndani ya klabu yao.
" Michezo ni amani na furaha na michezo si vurugu, uongozi wa Simba umetoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusiana na ubatili wa mkutano huo, tunapenda kuwaomba wanachama wetu wasiopenda fujo na vurugu kwenye michezo kukaa mbali na mkutano huo kwa vile vyombo vya dola vitaufuatilia.
"Uongozi hautajiingiza katika kutoa dhamana au msaada wa namna yoyote kwa yeyote ambaye atachukuliwa hatua na vyombo vya dola kutokana na kujihusisha na mkutano huo."alisisitiza Kamwaga.
Hata hivyo pamoja na kauli hiyo ya Kamwaga wanachama wa Simba kupitia kwa mmoja wa waratibu wa mkutano huo Mohamed Wandi wamesisitiza kufanyika kwa mkutano huo ambao utakuwa na ajenda mbili moja ikiwa ni mwenendo wa timu yao katika mashindano pamoja na kutokuwa na imani na uongozi wa Rage.
No comments:
Post a Comment