Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania,
Inspekta Jenerali Saidi Mwema kuomboleza kifo cha askari WP2494 Koplo
Elikiza ambaye amepoteza maisha kwa kugongwa na gari leo, Jumatatu,
Machi 18, 2013 saa saba mchana katika eneo la Bamaga, Dar Es Salaam.
WP
2494 Koplo Elikiza amegongwa wakati alipokuwa anamsimamisha dereva
mmoja aliyejaribu kujiunga, kinyume cha taratibu, mwishoni mwa msafara
rasmi wa magari ya Mheshimiwa Rais Kikwete, alipokataa kusimama baada ya
kupewa amri ya kusimama na askari huyo, na akamgonga.
Amesema
Rais Kikwete: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo
cha Koplo Elikiza ambaye nimejulishwa kuwa aligongwa na gari leo akiwa
kazini katika eneo la Bamaga, Dar Es Salaam, wakati alipokuwa anaongoza
msafara rasmi.”
“Ni
jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kuwa Koplo Elikiza amepoteza maisha
yake akiwa kazini kwenye utumishi wa jeshi lake na nchi yake, na wakati
taifa letu bado linaendelea kuhitaji sana nguvukazi yake. Tutaendelea
kumkumbuka kwa uaminifu wake kwa Jeshi la Polisi na kwa taifa lake la
Tanzania,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kifo
chake siyo tu kwamba ni pigo kwa nchi yetu, bali ni pigo kwa Jeshi la
Polisi nchini na ni pigo hasa kwa familia yake ambayo bado ilikuwa
inahitaji mapenzi, uangalizi na usimamizi wa mama.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirami kuomboleza
kifo hiki. Aidha, kupitia kwako nawatumia makamanda na askari wote wa
Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuondokewa na mwenzao. Vile vile, naomba
kupitia kwako unifikishie salamu za pole ya moyo wangu kwa familia ya
marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huuo mkubwa na naelewa
machungu yao.”
“Aidha,
napenda wajue kuwa naungana nao katika kumwombea marehemu, na pia
kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema poponi roho ya
Marehemu Koplo Elikiza. Amina.
No comments:
Post a Comment