RAIS Jakaya Kikwete
amesimulia maisha yake ya jeshini, huku akikumbuka namna alivyokamatwa
na mkuu wa jiko (afande ubwabwa) akiiba wali. Rais Kikwete alitoa
ushuhuda huo wakati akifunga mafunzo maalumu ya uongozi kwa wabunge na
kuzindua mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Hafla hiyo ilifanyika juzi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 832 KJ, kilichopo Ruvu, Kibaha mkoani Pwani, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria.
Rais Kikwete aliwakumbusha vijana hao kwamba yeye ni miongoni mwa watu waliochukua mafunzo ya JKT kambini hapo akiwa katika Operesheni Tumaini mwaka 1972.
Rais Kikwete alisema katika mafunzo hayo alijengwa vizuri, ingawa hadi leo bado anakumbuka matukio mawili ya kufurahisha na kusikitisha akiwa kambini hapo.
Alisema tukio la kwanza ambalo hawezi kusahau ni pale alipokamatwa akiiba wali na tukio jingine ni kuhusu kifo cha askari mwenzao aliyefariki dunia baada ya kukanyagwa na trekta.
“Nawashukuru kwa kunialika katika shughuli hii, nimetembelea na kujionea miradi mbalimbali inayoendelea kufanywa hapa kambini.
“Wakati tukiwa kule nilikuwa naangalia kwa makini, hasa nilikuwa naangalia lile bweni letu, sisi tuliokuwa Kombania A mwaka ule, nimepakumbuka ingawa sasa pamekarabatiwa vizuri.
“Yapo matukio mawili ninayoyakumbuka siwezi kuyasahu hadi leo wakati nikiwa hapa kambini…(kicheko) jeshi si mchezo, nawaeleza haya mjue maisha ya jeshi hayana mzaha.
“Nakumbuka namna nilivyokamatwa na bwana ubwabwa nikiiba wali kule katika bwalo la chakula,” alisema Rais Kikwete huku wananchi na askari wanafunzi (kuruta) waliokuwapo wakiangua kicheko.
Rais Kikwete aliendelea kusema. “Katika kombania yetu tulikuwa na mchezo siku zikipikwa nyama na wali tunaiba tunakwenda kuficha kisha baadaye tunakuja kula baada ya kazi.
“Sasa siku hiyo ilikuwa zamu yangu kuiba wali, kama kawaida nikachukua mestini zangu mbili nikachukua wali ili nikafiche, natoka tu nje, hamad! afande ubwabwa huyu hapa mlangoni (kicheko).
“Akaniambia piga magoti, huku nimeshikilia mestini zangu za wali. Akaniambia hivi! Brother maana alikuwa anapenda sana kuita brother, wewe ni form six (kidato cha sita) umekuja kuchukua mafunzo.
“Huko juu kuna makamu wa rais anaitwa Rashid Mfaume Kawawa, akisikia kwamba kuna kijana wa form six ameiba wali kambini atafurahi?
“Nikamwambia hapana, akasema kama hivyo ndivyo acha tabia hiyo, akanikanya nisiendelee na tabia ile. Nilikamatwa lakini nilifanikiwa kuondoka kwa huruma.
“Tukio la pili ninalokumbuka ilikuwa ni masuala ya kufundisha, tulikuwa tunakwenda Misugusugu kulikuwa na umwagiliaji katika skimu ya mpunga.
“Sasa tukiwa tunajiandaa zilifika habari kambini kwamba kuna askari mwenzetu amekanyagwa na trekta amefariki dunia, tukiwa bwenini nikapaza sauti ‘Stanley kuna habari gani, nasikia askari amekanyagwa na trekta’.
“Wakati napiga kelele, sikujua kumbe huyo ninayemwita ndiye aliyepatwa na janga hilo, tulienda kule barabarani kujua mazingira ya kifo yalikuwaje.
“Tulipofika pale tuliambiwa kwamba mwenzetu alikuwa amepanda trekta na alikaa kwenye madi gadi huku akila muwa, kwa bahati mbaya aliteleza akaanguka na kukanyagwa na tairi kubwa,” alisema Rais Kikwete huku watu wakisikitika.
Rais Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwaeleza vijana hao chimbuko la kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambapo vijana wanaomaliza kidato cha sita watajiunga na jeshi hilo kwa mujibu wa sheria kabla ya kujiunga na vyuo.
Rais Kikwete alisema JKT ilianzishwa mwaka 1963 na kwamba msingi wake mkuu ni kutoa fursa kwa vijana kujifunza na kujenga umoja wa taifa.
Akielezea historia ya jeshi hilo, Rais Kikwete alipinga madai ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidai kuwa wananchi walisomeshwa bure chini ya utawala wa awamu ya kwanza.
“Wazo la kuanzisha JKT lilianzia TANU Youth League, 10/07/1963 wazo lilitolewa na aliyekuwa katibu wake, Joseph Nyerere wakati huo, ndiye aliyependekeza JKT ianzishwe.
“Aprili 19, 1963 Baraza la Mawaziri liliridhia uanzishwaji wake. Sheria namba 64 ya mwaka 1966 ilitungwa na hapo JKT ilianza kupokea vijana wasomi wa elimu ya juu.
“Enzi zetu mafunzo ya JKT yalikuwa miezi 5 kambini, halafu miezi 18 kazini, baadaye unarudi kumalizia mwezi mmoja.
“Ilikuwa huwezi kuanza kazi bila kupitia JKT. Katika miezi yako 18 ya kazi, hapakuwa na ruhusa ya kuchukua mshahara wote.
“Unachukua asilimia 40 ya mshahara wako, asilimia 60 inayobaki Serikali inachukua kufidia gharama zake za mafunzo ya JKT, suala la kwamba watu walisoma bure katika nchi hii mimi silioni.
“Tumedhamiria kuboresha na kuongeza uwezo wa JKT ili iweze kutimiza wajibu wake. Jeshi hili lina wajibu mkubwa katika kuwajenga vijana na suala zima la uzalishaji mali,” alisema.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Kaimu Mkuu wa Kambi hiyo, Luteni Kanali Menas Mbele na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza.
Katika hatua nyingine, wabunge 25 wameshindwa kujiunga na mafunzo ya JKT yaliyofanyika katika kambi mbalimbali nchini, licha ya kujiandikisha.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wabunge 47 walijiandikisha, lakini wabunge walioripoti kambini ni 24 na waliohitimu mafunzo hayo ya wiki tatu ni 22 tu.
Wabunge waliohitimu mafunzo maalumu ya uongozi katika Kambi ya 832 KJ, Ruvu ni pamoja na Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
No comments:
Post a Comment