Friday, April 06, 2018
SALMAN KHAN AHUKUMIWA KUFUNGWA JELA KWA KOSA LA UWINDAJI HARAMU
Mahakama nchini India imemuhukumu
nyota muigizaji wa sinema za Bollywood Salman Khan, kifungo cha miaka
mitano jela kwa kuua aina mojawapo ya swala ambao ni adimu kupatikana
duniani mwaka 1988.
Mahakama hiyo iliyoko Jodhpur imemtoza faini ya rupia 10,000 ($154; £109) kwa kosa hilo.
Amepelekwa korokoroni na anatarajiwa kusalia huko kwa muda.
Khan aliwaua swala wawili kwa jina blackbucks, ambao hulindwa na kuhifadhiwa, Magharibi mwa jimbo la Rajasthan alipokuwa akiigiza filamu yake.
Thursday, April 05, 2018
CHADEMA WATAJA MAJINA 25 YA WAFUASI WAKE WANAOSHIKILIWA NA POLISI BILA KUPELEKWA MAHAKAMANI
Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa orodha ya majina
ya watu 25, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa wanaoshikiliwa na
Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam na kuwaagiza wanasheria wake
kuchukua hatua zaidi za kisheria kwa kuwasilisha maombi ya ‘Habeas
Corpus’, Mahakama Kuu, iwapo jeshi hilo halitawaachia au kuwafikisha
mahakamani watuhumiwa hao kama taratibu zinavyotaka.
Chama hicho kimesema kimefikia uamuzi huo, kutokana na tabia ya Jeshi
la Polisi kuendeleza utaratibu unaovunja haki na sheria kwa kuwakamata
watu na kuwashikilia mahabusu za Polisi kinyume na matakwa ya taratibu
za nchi.
Kati ya watu hao 25 wanaoshikiliwa na Polisi, mmoja ni Mjumbe wa Kamati
Kuu ya CHADEMA, John Heche, ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijiji huku
watu wengine 24 wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA
waliikamatwa juzi wakiwa maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakifuatilia hatma ya dhamana ya viongozi wakuu wa chama mahakamani
hapo.
BASI LA CITY BOYS LAGONGANA NA FUSO, 12 WAFARIKI, 46 WAJERUHIWA!
Basi la Kampuni ya City Boys lenye namba za usajili T983 DCE Scania limepata ajali ya kugongana na lori aina
ya Fuso lenye namba za usajili T486 ARB katika eneo la Makomero Tarafa na Wilaya Igunga Mkoa wa Tabora
usiku wa kuamkia leo na kusababisha vifo vya watu 12 na wengine 46
kujeruhiwa.
Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa wa Tabora, Insp Hardson,
amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa chanzo cha ajali
hiyo ni tairi la kulia la Fuso lilitumbukia kwenye mashimo mawili na
kusababisha tairi kupasuka na rimu kupinda hivyo likakosa mwelekeo na
kuligonga basi la City Boy uso kwa uso.
Insp Hardson amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali
ya igunga huku baadhi ya majeruhi wakipelekwa Hospitali ya Nkinga na
wengine Bugando Mwanza kwa ajili ya matibabu.
ALIEKUWA RAIS KUFUNGWA MIAKA 12 JELA
Mahakama ya rufaa nchini Brazil leo imeagiza aliekuwa rais wa nchi hiyo, Luiz Inacio Lula da Silva
kuwa ni sharti aanze kutumikia kifungo chake cha miaka kumi na mbili
gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika ufisadi.
Majaji sita kati ya kumi na mmoja wa
mahakama ya rufaa walipinga rufaa hiyo huku watano kati yao wakimuunga
mkono. Kesi hiyo imezua hali ya wasi wasi wa kisiasa nchini humo.
Lula amekutwa na hatia kutokana na uchunguzi wa muda mrefu wa sakata la rushwa linalojulikana kama ”Operation Car Wash" Lula aligundulika kukubali rushwa yenye thamani Euro laki 7.
WAZIRI ATAJA HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI KUFIKIA UCHUMI WA VIWANDA
Waziri
wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi akizungumza na wadau wa
utafiti wakati akifungua Warsha ya siku mbili kwa watafiti wa Tanzania
na kutoka nje iliyoandaliwa na Tasisi ya Utafiti ya REPOA jana jijini Dar
es Salaam.
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Balozi Amina Salim Alli akizungumza wakati anaongoza mjadala juu ya
Uchumi wa Viwanda kufikia 2025
Waziri
wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesisitiza Serikali
ya Awamu ya Tano inaendelea na hatua za kuhakikisha kunakuwepo
mazingira wezeshaji yatayofanikisha ujenzi wa viwanda nchini.
Prof.Kabudi
amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya
utafiti iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti ya REPOA ambapo mada kuu
ilikuwa kujadili kuelekea jamii inayoendeleza viwanda 2025 kwanini
ushindani ni muhimu.
Pia
kwenye warsha hiyo wadau wamejadili masuala ya kisera katika safari ya
Tanzania kuelekea kwenye uchumi mseto na shindani, ukiongozwa na viwanda, pamoja na kufikia nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama
inavyotarajiwa kwenye dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
ZITTO KUMPELEKA NONDO UHAMIAJI KUHOJIWA
Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe
amesema atamsindikiza kiongozi wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo
katika makao makuu ya uhamiaji Tanzania.
Hii ni baada ya taarifa iliotoka mtandao huo ambayo ilieleza kuwa Nondo alipata barua ya kuitwa na uhamiaji ili
'akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake'.
Taarifa
hizo zilisema 'afisa uhamiaji mkoa alitamka kuwa sheria inawaruhusu
kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka uraia wake. Na kuwa wanamashaka
na uraia wa Abdul Nondo,hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa
Tanzania'.
Wednesday, April 04, 2018
TAZAMA MUONEKANO MPYA WA MBOWE BAADA YA KUKAA MAHABUSU KWA SIKU SABA
Baada ya kukaa mahabusu kwa siku saba na
kusherehekea sikuu ya Pasaka wakiwa gerezani, Mwenyekiti wa Chadema
Taifa Mhe. Freeman Mbowe pamoja na vigogo wengine sita wa chama hicho
leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia kwa dhamana, baada ya
kukamilisha masharti.
KIKWETE AINGILIA KATI AFYA YA MZEE MAJUTO, HII HAPA AHADI YAKE
LICHA
ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume bado hali ya staa wa filamu za
Kibongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ ni tete ambapo Rais Mstaafu wa Awamu
ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’, amejitosa baada ya kumuona
alivyodhoofu kwa sasa.
JK na Mzee Majuto walikutana uso kwa
uso wikiendi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar ambako
kulikuwa na shughuli ya utoaji tuzo za filamu zilizojulikana kwa jina la
Tuzo za Kimataifa za Sinema Zetu ambapo walionekana wakiteta kwa dakika
kadhaa kabla ya kila mmoja akaenda kukaa kwenye siti yake.
Mzee Majuto alionekana akiwa amedhoofu
kwani aliingia ukumbini akitembea kwa msaada wa fimbo huku akionekana
kutokuwa mchangamfu kama ilivyo kawaida yake, hali iliyowahuzunisha
mashabiki wake waliokuwa ukumbini hapo.
AGNES MASOGANGE AKWEPA KWENDA JELA BAADA YA KULIPA FAINI
Msanii wa kupamba video za muziki (Video Queen), Agnes
Gerald ‘Masogange’ amekwepa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kulipa faini ya Sh. milioni 1.5.
Msanii maarufu nchini, Agnes Gerald maarufu Masogange alikutwa na hatia ya
kutumia dawa za kulevya na kuhukumiwa kwenda jela au kulipa faini.
Hakimu wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri, ametoa hukumu hiyo leo Aprili 3 na kuieleza mahakama kuwa Masogange katika kosa la kwanza amekutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin na kosa la pili kutumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.
“Hivyo katika kosa la kwanza, mahakama inamhukumu kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh1 milioni na kwa kosa la pili, amehukumiwa kwenda jela miezi 12 au kulipa faini ya Sh 500, 000,” amesema Hakimu Mashauri.
Februari 17 mwaka jana, aliyekuwa Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaeleza wanahabari kuwa Masogange amepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa iwapo anatumia dawa hizo za kulevya.
NUKUU SITA (6) MAARUFU ZA WINNIE MANDELA ENZI ZA UHAI WAKE
Winnie Madikizela-Mandela enzi za uhai wake.
Mwanasiasa na
mwanaharakati aliyepigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika
Kusini Winnie Madikizela-Mandela alifariki dunia Jumatatu akiwa na miaka
81.
Alikuwa mke wa zamani wa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini
Nelson Mandela lakini alikuwa na msimamo mkali zaidi kumshinda hata Bw
Mandela mwenyewe. Winnie alifahamika sana na wengi kama Mama wa Taifa.
Winnie alikuwa
nembo kuu ya vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, na ingawa sifa
zake ziliingia doa miaka ya baadaye, lakini bado alitambuliwa kama
mtetezi wa wanyonge.
Tuesday, April 03, 2018
MBOWE NA WENZIE KUACHIWA LEO...??!
Viongozi sita wa Upinzani nchini (CHADEMA) wanatarajiwa kuachiliwa kutoka kizimbani baada ya kulipa dhamana, siku ya Alhamisi.
Viongozi
hao akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe,
walishtakiwa kwa uchochezi, kuleta vurugu na kuandamana mwezi wa
Februari mwaka huu.
Alhamisi
iliopita, mahakama ya hakimu mkazi Kisutu iliwapatia dhamana viongozi
hao sita lakini kusema kuwa watasalia rumande hadi kesi leo tarehe 3
Aprili ambapo wataletwa mahakamani kukamilisha masharti ya dhamana.
Wanasiasa
hao hawakuletwa mahakamani katika uamuzi wa dhamana yao huku afisa wa
magereza akiiambia mahakama ni kutokana na gari lililotakiwa
kuwasafirisha kuja mahakamani hapo kuwa bovu.
Miongoni mwa
mashtaka waliyosomewa ni pamoja na maandamano yaliyosababisha kifo cha
mwanafunzi wa chuo cha NIT Akwilina Akwiline. Wanashtakiwa pia kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali wilayani Kinondoni shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Subscribe to:
Posts (Atom)