Stori: Makongoro Oging’
DUNIA haiishi vituko! Chacha Makenge (36) mzaliwa wa Kijiji cha
Kisangula, Mtukula, Serengeti mkoani Mara anaishi jijini Dar lakini
ndani ya handaki aliloligeuza chumba kwa miaka minne sasa, ni ajabu
lakini ni kweli.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni nje ya handaki hilo lililopo
mita chache kutoka majengo ya biashara ya Mlimani City, Makenge alisema
alichukua uamuzi huo baada ya rafiki yake (jina linahifadhiwa)
kumchomea nyumba na kuteketeza samani zote.
“Ilikuwa mwaka 2009 mwanzoni rafiki yangu huyo ndiye alinipa sehemu ya
kiwanja chake nijenge nyumba. Nikawa naishi hapo huku nikiendelea na
shughuli zangu za kila siku.
“Siku moja akabadili mawazo, akanitaka nihame katika eneo lake bila kunipa sababu, nilimwomba anipe muda nitafute pa kwenda.
“Julai 2009 akaja na polisi, akanikamata na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Stakishari, nilipowauliza kosa langu, hawakunieleza.
“Baada ya siku mbili majirani walikuja kuniona na kuniambia kwamba
nyumba yangu imechomwa moto na kila kitu kilichokuwa ndani kimeteketea,
aliyefanya hivyo ni rafiki yangu. Nilijisikia vibaya sana.