Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba
(pichani) amesema mchakato wa Katiba Mpya una vikwazo vingi na kwamba Katiba
haiwezi kupatikana mwaka 2014 kama Rais Kikwete alivyoahidi hivyo, kuna
haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Bara.
Hii ni mara ya pili kwa Lipumba kutoa kauli hiyo.
Mei mwaka huu, alitoa tamko kama hilo alipoonyesha wasiwasi wake kuhusu
upatikanaji wa Katiba Mpya akadai ni janja ya CCM kumwongezea muda Rais.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Lipumba
alisema kuwa amekuwa akiutafakari kwa kina mchakato wa Katiba Mpya kama
unaweza kukamilika mwaka 2014, lakini jibu linalomjia, hakuna.
Alitaja baadhi ya vikwazo ambavyo vinaweza
kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya kuwa ni Daftari la Kudumu la
Wapigakura kama halijaboreshwa na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho
vya utaifa ambavyo vitatumika kupigia kura hiyo.