Aidha, amesema kuwa vita aliyopo siyo kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, akitaja magenge ya watu wanaotaka urais 2015 na walioficha fedha nje ya nchi walioungana wakiona tatizo lao ni yeye hivyo kutaka kumwondoa bungeni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu, Zitto alisema kuwa hadi sasa bado hajapokea tuhuma 11 anazokabiliwa nazo, hivyo hajui makosa hayo na bado anasubiri akabidhiwe kwa maandishi.
Ana ugomvi gani na viongozi wenzake?
Alipotakiwa kueleza iwapo ana ugomvi na watu ndani ya Chadema, Zitto alisema kuwa huenda mambo hayo yanatokea kwa sababu mahasimu wake wa kisiasa wa ndani na nje wameamua kuungana na kupambana naye ili kumdhoofisha kisiasa kwa masilahi yao.
"Matatizo yaliyopo ni mafanikio yangu,
.... nadhani hii siyo vita kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya
watu wengi, pengine magenge ya watu wanaotaka urais na wale walioficha
fedha zao nje wamekaa pamoja wanaona tatizo lao ni Zitto... wanajua
siwezi kusemea nje maana sina kinga..., hivyo wanataka kuniondoa
bungeni..." alisema.
Aliongeza kuwa kwenye siasa
kinachohitajika ni kusimamia misingi, jambo alilosema binafsi amekuwa
akilifanya katika kipindi chake chote cha kisiasa.
Zitto alisema kuwa ni vyema wananchi
wakawapima wabunge wao kwa kazi wanazozifanya bungeni akibainisha kuwa
kati ya mwaka 2011 hadi 2013, yeye amewasilisha hoja nyingi nzuri zilizo
na mashiko ikilinganishwa na wabunge wenzake wanaomtuhumu kutumiwa na
CCM.