Aidha, amesema kuwa vita aliyopo siyo kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, akitaja magenge ya watu wanaotaka urais 2015 na walioficha fedha nje ya nchi walioungana wakiona tatizo lao ni yeye hivyo kutaka kumwondoa bungeni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu, Zitto alisema kuwa hadi sasa bado hajapokea tuhuma 11 anazokabiliwa nazo, hivyo hajui makosa hayo na bado anasubiri akabidhiwe kwa maandishi.
Ana ugomvi gani na viongozi wenzake?
Alipotakiwa kueleza iwapo ana ugomvi na watu ndani ya Chadema, Zitto alisema kuwa huenda mambo hayo yanatokea kwa sababu mahasimu wake wa kisiasa wa ndani na nje wameamua kuungana na kupambana naye ili kumdhoofisha kisiasa kwa masilahi yao.
"Matatizo yaliyopo ni mafanikio yangu,
.... nadhani hii siyo vita kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya
watu wengi, pengine magenge ya watu wanaotaka urais na wale walioficha
fedha zao nje wamekaa pamoja wanaona tatizo lao ni Zitto... wanajua
siwezi kusemea nje maana sina kinga..., hivyo wanataka kuniondoa
bungeni..." alisema.
Aliongeza kuwa kwenye siasa
kinachohitajika ni kusimamia misingi, jambo alilosema binafsi amekuwa
akilifanya katika kipindi chake chote cha kisiasa.
Zitto alisema kuwa ni vyema wananchi
wakawapima wabunge wao kwa kazi wanazozifanya bungeni akibainisha kuwa
kati ya mwaka 2011 hadi 2013, yeye amewasilisha hoja nyingi nzuri zilizo
na mashiko ikilinganishwa na wabunge wenzake wanaomtuhumu kutumiwa na
CCM.
"Je, mbunge anayetumika na Chama Cha
Mapinduzi anaweza kupeleka hoja ya kumng'oa Waziri Mkuu na kumshinikiza
Rais mpaka akasimamisha kazi mawaziri wanane? Je, mbunge anayetumika
anaweza kushikia bango watu wanaotorosha fedha nje ya nchi?" alihoji
Zitto.
Tuhuma za usaliti
"Sizijui hizo tuhuma 11 kwa sababu
nilichoelezwa kwenye kikao cha Kamati Kuu sicho kilichoelezwa na chama
kwenye mkutano wake na waandishi wa habari... hivyo sijui kabisa hizo
tuhuma zangu ni zipi mpaka sasa," alisema.
Alisema kuwa kwenye Kamati Kuu
alilaumiwa kwa masuala matatu. Akizitaja: "Nililaumiwa kuwa sifanyi kazi
za chama, la pili kuwa nimemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali
akague vyama kutokana na kuwa na nia mbaya na chama hicho. Tuhuma ya
tatu ni ile ya kukataa kupokea posho bungeni ambapo nadaiwa kulenga
kuwadhalilisha wabunge wenzangu."
Zitto alisema kuwa baada ya kuzijibu
tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kikao cha Kamati Kuu na katika mkutano
wake na waandishi wa habari, akashangazwa na tuhuma alizoziita mpya kuwa
anatuhumiwa kutokana na waraka ambao yeye hahusiki nao, licha ya
kutajwa kuwa mfaidika tu.
"Mimi sihusiki na waraka wowote, huo
unaodaiwa kusambazwa kwenye mitandao wala mwingine wowote... ni wajibu
wa chama kueleza mimi nahusikaje na waraka ule," alisema.
Madai ya Mwanasheria wa Chadema kuvunja Katiba
Zitto alisema jambo linalompa shaka
kuwa huenda suala lake limelenga kumdhoofisha kisiasa ni kitendo cha
mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu kuamua kuvunja katiba ya chama
hicho kwa makusudi.
Alifafanua: "Katiba ya chama
(Chadema), inasema kwamba kiongozi wa ngazi fulani ataondolewa kwenye
uongozi na ngazi iliyomchagua. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu la
Chama, siyo Kamati Kuu... sasa iweje Kamati Kuu iniondoe?"
Alisema kimsingi Kamati Kuu haina
mamlaka ya kumvua uongozi bali ina mamlaka ya kuweza kumsimamisha
uongozi kusubiri kikao kilichomchagua kufanya uamuzi wa kumwondoa katika
uongozi au kumrejesha.
Zitto alidai kuwa Lissu alisema uongo
kuwa hata Dk Wallid Kabourou aliondolewa uongozi na Kamati Kuu na kwamba
ukweli ni kuwa Dk Kabourou alijiondoa mwenyewe na kuhamia CCM na kwamba
hata Chacha Wangwe hakuondolewa na Kamati Kuu isipokuwa alisimamishwa
na kusubiri Baraza Kuu ambapo kabla ya Baraza Kuu kuketi alifikwa na
mauti.
Kwa nini hapokei posho?
Alipoulizwa ni kwa nini yeye hapokei
posho za wabunge alisema suala la posho siyo lake binafsi bali ni suala
la imani na msimamo wa chama hicho, ambao waliuweka wakati wa kampeni na
ni miongoni mwa mambo waliyowaahidi wapigakura wakati wa kampeni, hivyo
yeye anachofanya ni kutimiza tu ahadi.
Aliongeza kuwa wakati wa kampeni za
mwaka 2010, walikuwa wakiwaeleza wananchi kuwa wabunge wanapokea fedha
nyingi na kuwa wakichaguliwa watapunguza posho hizo na kwamba Chadema
ilipofanikiwa kushinda chama kilikubaliana watekeleze ahadi zile.
Alidokeza kwamba walikubaliana
kutekeleza kwa kuanza na mambo mawili moja likiwa kukataa kuchukua posho
za vikao, maana ni kinyume cha utaratibu na suala la pili ni kuacha
kutumia shangingi la Serikali ambalo linatumika na Kiongozi wa Upinzani
Bungeni.
Alisema katika kutekeleza uamuzi huo
Mbowe alitangaza hatua ya kurudisha shangingi na yeye (Zitto) kama
Waziri Kivuli wa Fedha akatangaza kuacha kupokea posho.
"Tulikubaliana wote tutekeleze hayo...
lakini wenzangu wakashindwa kuyatekeleza, na mwenzangu akalirudia gari
na analitumia mpaka sasa... kwangu mimi mafunzo niliyofundishwa kisiasa
ni kwamba unayoyasema, yatekeleze, wenzangu hiyo 'principal' ya
kutekeleza wanayoyasema hawana," alisema.
Kuhusu tuhuma kuwa anakataa posho
lakini anapokea rushwa kubwa kubwa, Zitto alisema iwapo kuna mtu aliye
na ushahidi na hilo aupeleke vyombo vya dola, wamshtaki na achunguzwe
kisha achukuliwe hatua.
Alisema mbali na posho, wabunge
wanaongoza kwa kupewa misamaha ya kodi mbalimbali ukiwemo msamaha wa
kodi ya uingizaji wa magari.
"Hii nayo tulikubaliana kuikataa... na
katika kulitekeleza hili, nilipoagiza gari langu nilikataa msamaha
nikalipa kodi hadi nilipoitwa na Kamishna wa Kodi na kuulizwa iweje
nilipe kodi wakati nina msamaha wa kodi nikamjibu kuwa ni suala la
'principal' tu," alisema.
Ruzuku
Kuhusu suala la ukaguzi wa ruzuku ya
chama, Zitto alisema yeye anapokuwa Mwenyekiti wa PAC anasimamia taifa,
hasimamii chama, hivyo kwa nafasi yake ya PAC na kamati nzima waliona
siyo halali vyama vya siasa kukaa bila kukaguliwa.
Alisema alipigania suala hilo tangu
mwaka 2011 alipomwandikia barua Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali kumuuliza kwa nini hakagui hesabu za vyama vya siasa wakati
sheria inataka vikaguliwe.
Je, ana shaka kuhusu matumizi ya ruzuku ndani ya Chadema?
"Nitaweza kusema jambo hilo kwa
uhakika baada ya ukaguzi kufanyika. Mpaka sasa hakuna chama ambacho
kimekaguliwa, hivyo inawezekana matumizi mabaya ya ruzuku yako CCM, CUF,
NCCR-Mageuzi, Chadema au yako katika vyama vyote...
"Haiwezekani kila mwaka sisi (wabunge)
tunaipigia kelele Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, haiwezekani
kila mwaka tunaipigia kelele Bodi ya Korosho, halafu vyama vya siasa
ambavyo vinapokea zaidi ya Sh29 bilioni kila mwaka, tukisema, tuonekane
wasaliti," alisema Zitto.
Chadema yajibu
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya
Zitto, jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa alisema kuwa
hawezi kulumbana na mtu kwa njia ya magazeti na kwamba kazi yake yeye ni
kufafanua Katiba, kanuni na miongozo ya Chadema pindi inapohitajika.
Anaripoti Ibrahim Yamola.
Alisema endapo kama kuna vifungu
katika Katiba, kanuni au miongozo vilivyokiukwa katika kufanya uamuzi
hayo vibainishwe na si kuongea katika magazeti bila kueleza makosa
yaliyofanyika.
"Mimi kazi yangu si kulumbana katika
magazeti, kama anaona (Zitto), kuna mambo yamekiukwa anatakiwa
kuyawasilisha sehemu inayohusika ili hatua zaidi zichukuliwe.
Wewe mwandishi umeoa? (Mwandishi;
hapana), ungekuwa umeoa ningekuuliza hivi; unaweza kutoa siri za ndani
za mke wako kwa watu wengine?," aliuliza Dk Slaa.
Akizungumzia kuhusu mikutano
inayoendelea mikoani, alisema haina lengo la kuwaeleza wananchi juu ya
uamuzi wa Kamati Kuu ya kuwavua madaraka Zitto na wenzake, bali ni
utekelezaji wa mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho uliofikiwa Junuari
mwaka huu.
"Mikutano hiyo imeanza tangu Aprili
mwaka huu, iko katika ngazi za vijiji na vitongoji vikikijenga chama na
wala si kwa dhana yoyote zaidi ya hiyo," alisema Dk Slaa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment