Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba wa mwaka 2013, huku kukiwa na ushindani wa maeneo mawili ambayo
baadhi ya wabunge walionyesha hofu.
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa
hati ya dharura kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo
yaliyofanyika Oktoba 15, mwaka huu, baina ya Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, baada ya muswada
wa awali kususwa na vyama vya upinzani bungeni.
Katika mjadala ulioanza juzi na
kuhitimishwa jana, wabunge wengi kutoka pande zote; CCM na upinzani
waliyaunga mkono mapendekezo ya Serikali, lakini kulikuwa na hofu kuhusu
idadi ya wajumbe watakaoteuliwa na Rais kuingia kwenye Bunge Maalumu na
suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Marekebisho hayo yameiweka kando Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo haitakuwapo baada ya kukabidhi rasimu ya
pili ya Katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete, Desemba 15, mwaka huu.
Uhai wa tume hiyo ni miongoni mwa
mambo yaliyozua ubishi baina ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa
wakitaka iendelee kuwapo na wale wa chama tawala na Serikali, ambao
walitaka iondoke kwa maelezo kwamba haitakuwa na kazi baada ya kukabidhi
rasimu kwa rais kama inavyoeleza sheria ya kuanzishwa kwake.