Na mwanahabari Bundala William
DHAMANA ya mbunge wa jimbo la Ukerewe,
Salvatory Machemli (CHADEMA) imefutwa na ameamuriwa na mahakama kwenda
rumande siku 14 kwa kuwa wadhamini wake wamekosa sifa baada ya
mshitakiwa na wadhamini wake watatu kushindwa kufika mahakamani ili
kuwezesha kesi inayomkabili kusikilizwa kama ilivyopangwa.
Pia, Mbunge huyo ametakiwa kuwasilisha vitambulisho vyake katika kituo cha polisi na amezuiliwa kutoka nje ya wilaya bila kibali cha mahakama.
Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
wilaya hiyo Faustine Kishenyi ametoa uamuzi huo leo baada ya upande wa
mashitaka kuomba mshitakiwa afutiwe dhamana.
Wadhamini ambao ni Shellifu Ngelezya, Max Mhogo na Konsolata Machemli wamepoteza sifa hivyo udhamini wao umefutwa.
Mwendesha mashitaka wa jeshi la
polisi, Inspekta Samweli Onyango amesema mshitakiwa kwa makusudi
ameshindwa kufika mahakani zaidi ya mara tano bila kutoa taarifa wakati
kesi yake ikitajwa.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, hakimu
huyo aliamuru mmoja wa wadhamini wake, Max Mhogo, awekwe rumande siku
saba na baada ya kutoka alitakiwa leo (Novemba 6) afike mahakamani hapo
na mshitakiwa pamoja na wadhamini wake.
Katika utetezi wake, Machemli amesema
ameshindwa kufika mahakani kama ilivyopangwa kwa sababu ya tarehe ya
kesi yake kuingiliana na vikao vya Bunge.
Kesi hiyo imeahirshwa hadi tarehe 20 mwezi huu .
Mbunge huyo anakabiliwa na kesi ya uchochezi.
Mwendesha mashitaka wa polisi, ASP
Denis Rwiza alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa
linalomkabili, Oktoba 23, 2011 katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara
wakati akiutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA.
Alisema mshitakiwa huyo kwa makusudi
aliwachochea wananchi kutenda kosa la shambulio kwa kuwaelekeza wachukue
uamuzi mgumu wa kuwazuia, hata kushambulia kwa silaha za jadi ikiwemo
marungu, mapanga na fimbo afisa yeyote wa polisi atakayekwenda kutafuta
watuhumiwa nyakati za usiku kisiwani hapo.
Katika maelezo yake, mwendesha
mashitaka huyo wa polisi alisema kipindi hicho ulikuwepo msako wa
watuhumiwa wa mauaji ya watu wanne waliouawa na wananchi Desemba 10,
2010 mbele ya maofisa wa polisi kwa tuhuma za ujambazi.
---
Taarifa wavuti.com ilizozipata jioni hii zinasema kuwa tayari Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe amemwandikia rasmi baruaKatibu wa Bunge kumjulisha juu ya jambo hili na wananchi wanaendelea kutafuta dhamana ili kukidhi masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na wadhamini watatu na hati tatu za nyumba.
Taarifa wavuti.com ilizozipata jioni hii zinasema kuwa tayari Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe amemwandikia rasmi baruaKatibu wa Bunge kumjulisha juu ya jambo hili na wananchi wanaendelea kutafuta dhamana ili kukidhi masharti yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na wadhamini watatu na hati tatu za nyumba.
Source: wavuti.com
No comments:
Post a Comment