Wakati Serikali imewasilisha muswada
wa marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Magazeti, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imepinga marekebisho ya sheria hiyo kwa madai
kuwa hayakufanyiwa tafakuri na utafiti.
Akiwasilisha maoni hayo bungeni jana,
Msemaji wa Kambi hiyo kuhusu Sheria, Tundu Lissu, alisema mapendekezo
hayo yamefikishwa bungeni bila kufanyia tafakuri au utafiti wowote.
"Mwanasheria Mkuu wa Serikali
angefanya utafiti kidogo tu angegundua kwamba kifungu cha 55 hakina na
hakijawahi kuwa na, sababu yoyote ya kuendelea kuwepo katika kanuni ya
adhabu,"alisema .
Alisema hiyo inatokana na kifungu
hicho hicho kutungwa upya, kwa maneno yale yale, kama kifungu cha 31 cha
Sheria ya Magazeti kwamba kifungu hicho hakikupaswa kuwepo kwa sababu,
makosa ambayo kifungu hicho kinafafanua hayako tena kwenye kanuni ya
adhabu na badala yake, yako katika Sheria ya Magazeti.
"Inaelekea katika fasta fasta ya
kupitisha muswada wa Sheria ya Magazeti, kifungu cha 55 kilisahauliwa
katika kanuni ya adhabu wakati vifungu vyote vinavyohusu makosa ya
uchochezi na kashfa ya kijinai vilipohamishiwa katika Sheria ya
Magazeti,"alisema Lissu.
Alisema kwa sababu hiyo kambi yake inapendekeza kwamba mapendekezo ya aya ya 47 ya muswada huo yaondolewe.
"Na sasa, kwa muswada huu, badala ya
kupendekeza sheria hii ifutwe kama ilivyokuwa kwa Sheria ya Shihata na
kama ilivyopendekezwa na Tume ya Nyalali, Serikali hii ya CCM inaliomba
Bunge lako tukufu kuiongezea makali zaidi," alisema.
Awali akiwasilisha muswada huo
bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema
muswada huo unapendekeza kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya
kuchapisha habari za uchochezi ama habari inayoweza kusababisha uvunjifu
wa amani.
Jaji Werema alisema hivi sasa adhabu
ya makosa hayo ni Sh 150,000 ambayo ni ndogo ikilinganishwa na madhara
ya kosa husika kwa jamii.
"Muswada unapendekeza katika ibara ya
40 na 41 kuwa vifungu hivyo virekebishwe kwa lengo la kuongeza adhabu ya
faini kwa makosa hayo ili adhabu hiyo isizidi Sh5 milioni," alisema.
Jajin Werema alisema marekebisho hayo
yanalenga katika kutekeleza azimio la Bunge katika mkutano wa 11 kikao
cha 21, ambapo pamoja na mambo mengine Serikali ilitakiwa kupitia sheria
zilizopo ili kuona kama zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za
uchochezi.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,
iliunga mkono marekebisho hayo yanayolenga kuongeza adhabu kwa makosa ya
kutumia lugha za matusi na uchochezi unaoweza kusababisha machafuko.
Wanasheria walonga
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na
gazeti hili wamesema marekebisho yanayofanywa na Bunge, hayana maana kwa
sasa na badala yake, sheria nzima inapaswa ifutwe kwa sababu
hailengi kujenga bali kuvibana vyombo vya habari.
Mwanasheria wa kujitegemea, Aloyce
Komba alisema ni wakati mwafaka wa Serikali kurejea na kuridhia
mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali ya kuzifuta sheria 40 zilizoainishwa
na tume yake.
Alisema miongoni mwa sheria 40 zilizopendekezwa kufutwa na Jaji Nyalali, ni sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ofisa Habari wa Mpango wa Kujitathmini
Kiutawala Bora Afrika, Wakili Hamza Abbas, alisema endapo Serikali
inafanya marekebisho ya vifungu ambavyo havitajwi katika kesi au shauri
lililopo mahakamani, inakuwa haijaingilia mahakama.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment