Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba wa mwaka 2013, huku kukiwa na ushindani wa maeneo mawili ambayo
baadhi ya wabunge walionyesha hofu.
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa
hati ya dharura kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo
yaliyofanyika Oktoba 15, mwaka huu, baina ya Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, baada ya muswada
wa awali kususwa na vyama vya upinzani bungeni.
Katika mjadala ulioanza juzi na
kuhitimishwa jana, wabunge wengi kutoka pande zote; CCM na upinzani
waliyaunga mkono mapendekezo ya Serikali, lakini kulikuwa na hofu kuhusu
idadi ya wajumbe watakaoteuliwa na Rais kuingia kwenye Bunge Maalumu na
suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Marekebisho hayo yameiweka kando Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo haitakuwapo baada ya kukabidhi rasimu ya
pili ya Katiba hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete, Desemba 15, mwaka huu.
Uhai wa tume hiyo ni miongoni mwa
mambo yaliyozua ubishi baina ya wabunge wa Kambi ya Upinzani waliokuwa
wakitaka iendelee kuwapo na wale wa chama tawala na Serikali, ambao
walitaka iondoke kwa maelezo kwamba haitakuwa na kazi baada ya kukabidhi
rasimu kwa rais kama inavyoeleza sheria ya kuanzishwa kwake.
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria,
Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani alisema kuvunjwa kwa
tume kutaathiri utekelezaji wa vifungu vingine vya sheria hivyo, ikiwa
ni pamoja na kile kinachotaka Mwenyekiti wa Tume, makamu wake au
makamishna kuitwa kwenye Bunge la Katiba kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa
mambo yatakayozua utata.
Kwa msingi huo kambi hiyo ilipendekeza
tume hiyo isivunjwe na wajumbe wake waingie katika Bunge Maalumu la
Katiba kama wataalamu wa kulisaidia Bunge hilo, lakini wasiwe na haki ya
kushiriki uamuzi kwa maana ya kupiga kura.
Hata hivyo, mapendekezo hayo na
mengine ya aina hiyo yaliyoletwa na nyaraka za marekebisho (schedule of
amendments) wakati Bunge lilipoketi kama kamati kupitia muswada huo
vifungu kwa vifungu yalitupwa, hivyo kuweka ukomo wa Tume ya Warioba
mara baada ya kukabidhi rasimu ya pili kwa Rais Kikwete, Desemba 15,
2013.
Wakati wakivutana, Lissu aliwarushia
lawama wabunge wa CCM kuwa wanawakataa wajumbe wa tume kwa sababu
ilipendekeza serikali tatu ambazo wao hawazitaki.
Lissu alisema kwa kauli na vitendo
hivyo, vilionyesha wazi kuwa CCM kinamsaliti Waziri Mkuu Mstaafu Jaji
Joseph Warioba ambaye amefanya kazi kubwa na ya weledi kiasi cha
kupongezwa na Rais Kikwete.
Katika majibu yake kwa wabunge, Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alipinga na kueleza kuwa hata kama
wabunge wangetaka Tume ya Warioba iwe ni sehemu ya Bunge la Katiba,
hakuna umuhimu huo.
Chikawe alifafanua kuwa sheria inaeleza wazi kuwa kipindi cha uhai wa tume hiyo kinakoma baada ya kukabidhi rasimu tu.
Bunge la Katiba
Kulikuwa na hoja iliyotaka wabunge
watakaoteuliwa na raia kutoka katika makundi idadi yao iongezwe hadi
292, kutoka wajumbe 201 waliokuwa wamependekezwa.
Itakumbukwa kuwa Serikali ilishaongeza
idadi hiyo ambayo awali ilikuwa ni wajumbe 166 hadi kufikia wajumbe 201
ambao hata hivyo bado baadhi ya wabunge walipinga kuwa ni wachache.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
(Chadema) alitoa hoja hiyo na kueleza sababu za kutaka idadi hiyo ambapo
alisema kuwa makubaliano ya awali yalikuwa ni lazima kuwepo na theluthi
mbili ya wabunge hao.
"Awali pendekezo la Serikali lilikuwa
ni kupata mbili ya tatu ya wabunge wote, mheshimiwa mwenyekiti, ikiwa
sasa wabunge wa Bunge la Jamhuri pamoja na Wawakilishi tunafika jumla
yetu 438, Serikali haioni kuwa mbili ya tatu ni watu 292 ni kwa nini
wasikubali wazo letu," alihoji Mnyika.
Hoja hiyo ilileta mvutano huku wabunge
kutoka Chama Cha Mapinduzi wakilalamikia kuwa kuongeza idadi ni sawa na
kuongeza gharama za bunge.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu
Nchemba alisema kuwa kinachompa wasiwasi Mnyika ni kutokana na ukweli
kuwa wanaotakiwa kushiriki bunge hilo wengi wanatoka Chama Cha
Mapinduzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti
Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alipinga pendekezo la Mnyika na kudai kuwa
halikuwa na mashiko yenye masilahi kwa Taifa.
"Mheshimiwa Mwenyekiti,
anachokizungumza Mheshimiwa Mnyika hakina mashiko kwani suala la
kuongeza idadi ya wajumbe halipaswi kuingizwa, sisi tuliomo humu ndani
tumechaguliwa na wananchi wote sawa na hao anaopendekeza Mnyika, kwani
shida ni nini tena?" alihoji Bulaya.
Wasomi na wanasheria wanena
Akizungumzia hatua hiyo iliyopitishwa
na Bunge, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Tolly Mbwete alisema uamuzi
huo umezingatia busara na utasaidia kuepusha wajumbe wa Bunge la Katiba
kulazimishwa kukubaliana na mawazo yaliyopo kwenye rasimu.
Alisema kuwa ni vyema wajumbe hao
wakaingia ndani ya Bunge hilo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi au maelezo
pale itakapobidi, lakini wasishiriki kama wajumbe wa Bunge hilo.
"Naona uamuzi huu umefanyika kwa
busara, kwani wajumbe wa tume tayari wameshatoa mawazo yao endapo
wataingia pia kwenye Bunge la Katiba kuna hatari ya kulazimisha mawazo
hayo kupitishwa na hatimaye kuandika kwenye Katiba ila endapo
watahitajika kutoa ufafanuzi waruhusiwe kuingia."
Naye Profesa Abdalla Safari ambaye ni
mwanasheria alisema hakuna sababu ya wajumbe hao kuingia kwenye Bunge la
Katiba kwa kuwa mawazo yao wameshayatoa kwenye rasimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema
uamuzi huo haukupaswa kupitishwa kwa kuwa wajumbe wa Tume ya Warioba
ndio walioandaa rasimu, hivyo walipaswa kushiriki katika Bunge hilo kwa
ajili ya kuiwasilisha na kuitolea ufafanuzi.
Aliongeza kuwa Serikali haina mamlaka
ya kuuwasilisha muswada huo kwa kuwa tume hiyo ilichaguliwa
kuwawakilisha wananchi, hivyo kutoshiriki katika Bunge hilo kunawanyima
haki ya msingi Watanzania ambao ndiyo wanahusika na katiba hiyo.
"Tume ya Warioba inasimama badala ya
wananchi kuwanyima haki ya kushiriki katika Bunge hilo kunamaanisha
kuwatoa wawakilishi wa wananchi ambao wana uwezo wa kusimamia na kutolea
ufafanuzi wa rasimu ambayo itatengenezewa Katiba ya Tanzania," alisema
Dk Bisimba.
No comments:
Post a Comment