NA MWANDISHI WETU
HATUA ya Marekani kudaiwa kufuatilia
mawasiliano ya viongozi wa nchi washirika wake wa karibu, sasa ni wazi
imeiacha Tanzania katika wingu la shaka, kama viongozi wake nao
wanafuatiliwa kwa namna ile ile inayoelezwa na viongozi wa Ulaya. Shaka
hiyo inatokana na urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na
Marekani, ambapo kwa nyakati tofauti, marais watatu wa taifa hilo kubwa
duniani wamepata kuzuru nchini.
Kauli tofauti zilizotolewa ndani ya
wiki hii na majasusi wa mataifa makubwa duniani, ikiwemo Marekani na
Uingereza, wakati wakizungumzia madai ya Marekani kufuatilia mawasiliano
ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kwamba nchi zote duniani
zinachunguzana, ndiyo ambayo baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai
kuwa Tanzania bila shaka haiwezi kukwepa kufuatiliwa.
Mbali na hiyo, kauli ambayo imepata
kutolewa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA, Edward Snowden,
kwamba ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi
na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu, bali hata marafiki na
waitifaki wa karibu kabisa na nchi hiyo, ndiyo ambayo inajenga mazingira
ya Tanzania nayo kuwemo kwenye orodha hiyo ya kufuatiliwa.
Marais watatu wa Marekani, kwa nyakati
tofauti wamepata kuzuru nchini. Maraisi hao ni pamoja na Bill Clinton,
George W. Bush na Barack Obama, ambaye alitembelea nchini mwezi Julai,
mwaka huu.