Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba
wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili
achukue mikoba ya Abdalla Kibadeni.
SIMBA itaanza mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu Bara, Januari 26 mwakani dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa na kocha mpya, Mwanaspoti linaweza
kuthibitisha.
Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba
wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili
achukue mikoba ya Abdalla Kibadeni.
Williamson (52), ni straika wa zamani wa West Bromwich Albion na katika mechi 53 aliyoichezea timu hiyo alifunga mabao 11.
Williamson, ambaye ni raia wa Scotland
alijiunga na Gor Mahia msimu huu na tayari ameipa ubingwa wa Ligi Kuu
Kenya ikiwa ni miaka 18 tangu timu hiyo itwae ubingwa wa Kenya mwaka
1995.
Williamson, ambaye alikuwa kocha wa
timu ya taifa ya Uganda na kuipa ubingwa wa Kombe la Chalenji mara nne,
ni kocha anayesifika kutokana na kufundisha soka la kisasa kwa timu
kushambulia na kukaba kwa pamoja.
Habari kutoka makao makuu ya Simba,
barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam zinasema kuwa maofisa kadhaa
wa klabu hiyo wameanza mazungumzo na kocha huyo.
Habari hizo zinasema kuwa Simba ina
asilimia kubwa ya kumnasa kocha huyo kwa sababu alikuwa na mkataba wa
mwaka mmoja tu Gor Mahia na kwamba analipwa kidogo.
Simba imeamua kuingiza nguvu zake kwa
kocha huyo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo ambayo
inashika nafasi ya nne katika ligi, lakini kubwa zaidi ni kutokana na
benchi la ufundi kushindwa kudhibiti nidhamu kwa wachezaji na kucheza
mpira wa hovyo uwanjani.
Hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa
tayari kulizungumzia hilo, licha ya karibu wote kukiri kuwa
hawaridhishwi na jinsi timu hiyo inavyocheza.
Williamson aliteuliwa na Shirikisho la
Soka Uganda (Fufa) kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo 'The
Cranes' Agosti 19, 2008 akichukua nafasi ya Csaba Laszlo, aliyekuwa
amejiuzulu Julai 2008 baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Hearts
inayoshiriki Ligi Kuu Scotland.
Akiwa na kikosi cha Uganda, Williamson ameshinda mataji manne ya Kombe la Chalenji mwaka 2008, 2009, 2011 na 2012.
Uganda nusura itinge katika fainali za
Mataifa ya Afrika 2013, lakini ilipoteza mchezo wake wa mwisho wa
kufuzu baada ya kupigiana penalti na Zambia.
Hata hivyo, Fufa ilimtimua kazi
Williamson Aprili 8, mwaka huu na nafasi yake ikachukuliwa na Kocha wa
Serbia Sredojevic Milutin 'Micho', ambaye alikuwa ametimuliwa timu ya
taifa ya Rwanda.
Julai 5, mwaka huu, Williamson
alijiunga na Gor Mahia ya Kenya akichukua nafasi ya Zdravko Logarusic wa
Croatia, ambaye alikuwa amefukuzwa siku tisa za nyuma yaani Juni 25
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment