NA MWANDISHI WETU
HATUA ya Marekani kudaiwa kufuatilia
mawasiliano ya viongozi wa nchi washirika wake wa karibu, sasa ni wazi
imeiacha Tanzania katika wingu la shaka, kama viongozi wake nao
wanafuatiliwa kwa namna ile ile inayoelezwa na viongozi wa Ulaya. Shaka
hiyo inatokana na urafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na
Marekani, ambapo kwa nyakati tofauti, marais watatu wa taifa hilo kubwa
duniani wamepata kuzuru nchini.
Kauli tofauti zilizotolewa ndani ya
wiki hii na majasusi wa mataifa makubwa duniani, ikiwemo Marekani na
Uingereza, wakati wakizungumzia madai ya Marekani kufuatilia mawasiliano
ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kwamba nchi zote duniani
zinachunguzana, ndiyo ambayo baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai
kuwa Tanzania bila shaka haiwezi kukwepa kufuatiliwa.
Mbali na hiyo, kauli ambayo imepata
kutolewa na mfanyakazi wa zamani wa shirika la NSA, Edward Snowden,
kwamba ujasusi huo wa Marekani haufanywi dhidi ya watuhumiwa wa ujasusi
na wakazi wa nchi zenye ugomvi na Marekani tu, bali hata marafiki na
waitifaki wa karibu kabisa na nchi hiyo, ndiyo ambayo inajenga mazingira
ya Tanzania nayo kuwemo kwenye orodha hiyo ya kufuatiliwa.
Marais watatu wa Marekani, kwa nyakati
tofauti wamepata kuzuru nchini. Maraisi hao ni pamoja na Bill Clinton,
George W. Bush na Barack Obama, ambaye alitembelea nchini mwezi Julai,
mwaka huu.
Ni kutokana na hilo, hulka ya vyombo
vya usalama vya Marekani kuhakikisha usalama kwa viongozi wao haiwezi
kuwatenga na suala zima la kufanya udukuzi kwa nchi ambazo zina ushirika
nao, lakini pia viongozi wake wanatembeleana.
Kwa muktadha huo, tayari baadhi ya
wachambuzi waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina
yao gazetini wanasema kuwa uwezekano wa Marekani kufuatilia mawasilino
ya viongozi wa hapa nchini, akiwemo Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ni
mkubwa na ni jambo lisilo la kushangaza.
Wachambuzi hao wanazilinganisha
taarifa za sasa za udukuzi wa mawasiliano unaodaiwa kufanywa na Marekani
na mchezo ambao ulipata kufanywa huko nyuma na mtandao wa Weakleaks,
dhidi ya Tanzania.
Mtandao huo umepata kuwagusa viongozi
wa serikali, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, kutokana na taarifa za siri
ilizodai kuzinukuu kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa Marekani
nchini.
Kwa takribani wiki mbili sasa,
Marekani imejikuta katika mzozo wa kidiplomasia na baadhi ya mataifa ya
Ulaya, baada ya kuibuka madai kuwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel,
simu zake zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu muongo mmoja sasa.
Kama ilivyo kwa Tanzania na pengine zaidi ni kwamba Marekani na Ujerumani, zimekuwa na ushirika wa karibu kwa muda mrefu sasa.
Juni mwaka huu, mwanausalama aliyeasi
wa Marekani, Edward Snowden, alitoboa siri ya idara za usalama nchini
humo kwamba zimekuwa zikifuatilia mawasiliano ya simu na barua pepe kwa
watu mbalimbali duniani kote, wakiwamo viongozi wenye ushirika wa karibu
na taifa hilo.
Hata hivyo, Marekani imekana kufanya
udukuzi kwa namna ambayo imetafsiriwa na baadhi ya washirika wake na
badala yake imedai kuwa udukuzi ambao imekuwa ikiufanya ni wa kawaida
kwa ajili ya usalama na kwamba wamekuwa wakirejesha taarifa zote kwa
nchi husika.
Mkurugenzi wa Idara ya Usalama ya
Marekani, James Clapper, alisema upelelezi wa Marekani katika mataifa ya
kigeni huwa haufanywi kiholela.
"Nia ya viongozi ndiyo moja ya sababu
kuu ya kwanini tunafanya upelelezi na kuutathmini...washirika wa
kimataifa wa Marekani pia huchunguza maofisa wa Marekani na mashirika
mengine kama sehemu ya mipango ya serikali,"alisema Clapper.
Chanzo:Mtanzania mtandaoni
No comments:
Post a Comment