Padri Joseph Magamba wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui Zanzibar aliyemwagiwa tindikali akisaidiwa kushuka kwenye ndege na Padri Thomas Assenga(kushoto) wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Zanzibar baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kuelekea katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.Picha na Fidelis Felix
Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang'amba kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, imebainika kuwa alitishiwa kuuawa miezi mitatu kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa
maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo
alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka
visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.