Padri Joseph Magamba wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui Zanzibar aliyemwagiwa tindikali akisaidiwa kushuka kwenye ndege na Padri Thomas Assenga(kushoto) wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Zanzibar baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kuelekea katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.Picha na Fidelis Felix
Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang'amba kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, imebainika kuwa alitishiwa kuuawa miezi mitatu kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa
maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo
alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka
visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Dk Shein alisema Polisi inatakiwa
kuongeza nguvu za uchunguzi ili kukabiliana na matukio ya kikatili ya
umwagaji wa tindikali, yanayoshamili visiwani humo hivi sasa.
"Hatuwezi kuviacha vitendo hivi
viendelee ... ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika
ili sheria ichukue mkondo wake," alisema Dk Shein.
Dk Sheni alisema, kitendo hicho ni cha
kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya
Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo
mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang'amba alitolewa vitisho na
mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee
cha Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo,
kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani
ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
"Unajua kawaida ya watu wa Zanzibar
hufanya mazoezi barabarani, sasa kipindi anapita eneo hilo katika
kilima, kuna mtu alimwambia atamfanyia kitu kibaya ambacho hatujui ndiyo
hiki au la," alisema Padri Assenga na kuongeza:
Alisema Juni mwaka huu mara baada ya kupewa vitisho hivyo alikwenda kutoa taarifa kwa Sheha wa eneo hilo na kituo cha polisi.
"Mara baada ya kutolewa vitisho hivyo
Juni mwaka huu, alichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwa mkuu wa
eneo hilo (Sheha) na kituo cha polisi."
Akielezea tukio la kumwagiwa tindikali
Padri Mwang'amba, alisema alimwagiwa saa 9:45 alasiri juzi wakati
akizungumza na simu nje ya internet cafe iliyopo eneo la Mlandege.
Padri Assenga alisema kabla ya
kumwagiwa tindikali, Padri huyo alikuwa ndani ya internet akitoa
'photocopy' za nyaraka. Alipokuwa akitoa 'photocopy' (nakala) alipigiwa
simu na mtu ambaye anamfahamu hivyo ikabidi atoke nje kuongea naye,
lakini alivyokuwa akiongea alimwona kijana akija na kikopo alichokishika
mkononi na kummwagia na kukimbia kuelekea katika mitaa ya eneo hilo,"
alisema Padri Aseenga.
Alisema mara baada ya hapo, alipelekwa
katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, kwa matibabu baada ya kujeruhiwa
usoni, kifuani na mikononi ambapo hivi sasa afya yake inaendelea vizuri.
Naye , Msemaji wa Jeshi la Polisi, Zanzibar Mohamed Muhina alisema, hana taarifa hizo za vitisho na kuahidi kulifanyia kazi.
"Tukio limetokea mchana kweupe na watu
walikuwapo lakini wananchi wamekuwa hawatupi ushirikiano hivyo
tunawaomba kutupa ushirikiano ili kukomesha vitendo hivi," alisema
Muhina.
Tukio lilivyokuwa
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo,
Padri Mwang'amba alisema kwamba lilitokea nje ya duka linalotoa huduma
za mawasiliano ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la
Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na
kumwagia tindikali.
Padri Mwang'amba akimweleza Dk Shein
kuwa hali yake ni nzuri na anaweza kuona vizuri, lakini anatarajia
kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua katika sehemu za usoni na
machoni mwake.
"Hali yangu ni nzuri lakini natarajia
uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi," alisema Padri Mwang'amba na
kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake kwa kutoathirika sana.
Uwanja wa Ndege
Katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Julius Nyerere, Kiongozi huyo aliwasili saa 4.16 asubuhi na ndege ya
Shirika la Costal akiongozana na Padri Assenge.
Kiongozi huyo aliyekuwa akitembea
taratibu, huku akijitahidi kujifunika mwili wake na kanga kuzuia mwanga
wa Jua kutokuathiri zaidi mwili wake ulioathiriwa na tindikali.
No comments:
Post a Comment