Baadhi ya wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam wamedai kuwepo kwa wafanyakazi ambao ni wahamiaji haramu katika uwanja huo, ambao wamekuwa wakipewa nafasi nyeti katika mamlaka hiyo.
Aidha, wameeleza kuwa wahamiaji hao haramu pia wamekuwa wakipatiwa vitambulisho nyeti kama watanzania halisi.
Wafanyakazi walimueleza Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana alipofanya ziara uwanjani hapo na kuzungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) katika uwanja huo.
Mfanyakazi Dominic Bomani alisema
licha ya juhudi za serikali kuwaondoa nchini wahamiaji haramu, kiwanja
hicho cha ndege kimekuwa chimbuko la wahamiaji hao ambao wamekuwa
wakipewa nafasi nyeti.
Aliomba serikali kusaidia katika
kuwabaini na kuwaondoa wahamiaji hao ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi
hizo ziweze kushikiliwa na watanzania ambao wako wenye sifa stahili.
Dk Mwakyembe alishukuru kwa taarifa
hizo na kuahidi kufanyia kazi huku akimtaka mfanyakazi huyo kufika
ofisini kwake ili kumpa taarifa zaidi.
"Nashukuru kwa taarifa hizo kwani
hatukuwa nazo na ninaahidi kuanza kuzifanyia kazi na kutoa majibu yake
haraka kuanzia Jumatatu (kesho)," alisema.
Kuwepo kwa wafanyakazi wahamiaji haramu kumeonekana huenda ikawa ndiyo sababu ya matukio
yaliyotokea katika uwanja huo ya kupitisha dawa za kulevya kutokana na wahusika kutokuwa na uzalendo na taifa hili.
Katika siku za hivi karibuni serikali ilianzisha operesheni za kuwarejesha makwao wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali.
Operesheni hiyo iliyobatizwa jina la
'Kimbunga' iliahidiwa na Rais Jakaya Kikwete akiwa mkoani Kagera hivi
karibuni, baada ya kuwataka wahamiaji haramu kurejea walikotoka au
kufuata taratibu za kisheria za kuishi nchini, huku akionya kinyume cha
hapo, kwa kuwa miongoni mwao wanajihusisha na ujambazi, watasakwa
misituni, majumbani na hata ardhi itachimbuliwa, kutafuta silaha
walizozifukia ilianza kwa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumalizika
katika mikoa ya Geita, Kagera Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian
Massawe, aliyekuwepo katika mkutano huo wa Rais Kikwete alisema ni
wahamiaji haramu 11,601 tu walioondoka wakati uongozi wa mkoa huo,
ulitarajia wahamiaji haramu kati ya 52,000 na 53,000 waondoke.
Mkuu wa Operesheni hiyo ya Kimbunga,
Kamanda Simon Sirro alisema tangu operesheni hiyo ianze, wahamiaji
haramu 1,851 wamekamatwa, ng'ombe 1,763 na silaha za moto saba, bunduki
za kienyeji maarufu magobori sita na shotgun moja katika mikoa lengwa ya
Kagera, Kigoma na Geita.
Katika Mkoa wa Kigoma, operesheni hiyo
imefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 885, silaha mbili, gobori moja na
shotgun moja na ng'ombe 200.
Mkoani Geita, wahamiaji haramu 246
wamekamatwa, magobori matatu, ng'ombe 240, sare za Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kibuyu cha maji cha jeshi hilo.
Katika mkoa wa Kagera, wamekamata
wahamiaji haramu 750, magobori mawili na ng'ombe 1,323. Mbali na silaha
hizo zilizokamatwa, silaha zingine 65 zimesalimishwa; SMG tatu, shotgun
10 na magobori 52.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, silaha
nyingi zilisalimishwa katika wilaya ya Biharamulo na ndizo zilizokuwa
zikitumika katika utekaji na unyang'anyi katika mapori wilayani humo.
Jijini Dar es Salaam, Operesheni
Kimbunga kwa ajili ya wahamiji haramu kwa mujibu wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, hadi jana wahamiaji 465 kutoka mataifa
17 wakiwamo walimu wanaofundisha shule za michepuo ya Kingereza
wamekamatwa.
Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Grace Hokororo alitaja waliokamatwa kuwa ni Warundi 181, Wakongo
38, Wanyarwanda watano, Waganda 16, Wakenya 38, Wapakistani sita,
Wasomali 28, Wanigeria 12, raia wanane wa Msumbiji, 114 wa Malawi,
wawili wa Cameroon na 10 wa India.
Aidha, walikamata raia watatu wa Uturuki, watatu wa Comoro, mmoja wa Afrika Kusini, mmoja wa China na mmoja wa Burkina Faso.
Alisema wahamiaji hao wengi wao ni
vijana na wamekuwa wakijifanya walimu wa shule za michepuo ya Kingereza,
lakini hawana taaluma hiyo, isipokuwa wanakijua Kingereza na wengine ni
wauza kahawa, wafanyakazi wa ndani, walinzi, watunza bustani, wauza
matunda na maji. --- HabariLeo, JUMAPILI
No comments:
Post a Comment