Bunge limeingia katika mzozo
mwingine na Chadema baada ya kudaiwa kutoa ripoti polisi likitaka
wabunge 28 wa upinzani waitwe ili wahojiwe katika Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na fujo zilizotokea bungeni
Februari, mwaka huu. Hata hivyo, chama hicho kikuu cha upinzani kupitia
kwa
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu, kimepinga hatua hiyo
kikisema kamati hiyo haipo kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 113(7) kwa
kuwa imemaliza muda wake tangu Februari 8, mwaka huu na Spika hajaunda
nyingine.
Hata hivyo, madai hayo ya Lissu yamepingwa vikali na Naibu Spika, Job
Ndugai ambaye amesema kamati hiyo pamoja na nyingine mbili za Uongozi
na ile ya Kanuni zinatambulika mpaka zitakapoundwa nyingine... “Hizo
tatu ni ‘ongoing’ (zinaendelea) zisipokuwapo, basi Bunge hakuna.”
Mvutano huo ni wa pili katika siku za karibuni baada ya ule uliotokea
katika Kikao cha Bunge la Februari baada ya Wabunge wa Chadema kuzua
tafrani zilizosababisha kukatishwa kwa kikao kimoja cha Bunge hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Lissu alisema yeye na wabunge wenzake
wapatao 28 watafika mbele ya kamati hiyo lakini wamekubaliana kuwa
hawako tayari kuhojiwa nayo.
Mbali ya Lissu, jana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia
mkutano wa hadhara mjini Musoma alisema wabunge wa chama chake
hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo.
Lissu alisema njia iliyotumika kuwaita mbele ya kamati hiyo kwa
kupitia polisi ni kinyume na utaratibu.
“Utaratibu uliotumika ni haramu kwa kuwa polisi ndiyo wametumika
kutujulisha kwamba tunatakiwa tufike mbele ya kamati hiyo, kutumiwa
ujumbe wa polisi si sawa kwani utaratibu wa Bunge unajulikana,” Lissu
alisema na kuongeza:
“Kamati iliposema bungeni kuwa mimi na wenzangu watatu ni vinara wa
fujo ilituhukumu tayari, hivyo kisheria wale wengine waliobaki walikuwa
hawana makosa kwa mujibu wa sheria zetu.”
Ilidaiwa kwamba Ofisi ya Bunge iliiandikia Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi kutaka kuwaelekeza makamanda wake kufikisha taarifa hizo.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema hakuwa
na taarifa hizo na kuahidi kufuatilia.
Alipoulizwa kuhusu wabunge hao kuitwa kwa kutumia polisi, Ndugai
alisema hakuwa na taarifa hiyo na kuelezea wasiwasi kwamba suala hilo
limefikia hatua hiyo.
“Sidhani kama imefikia huko (kutumia polisi kuwaita wabunge), kwani
kamati ina utaratibu wake wa kumwita mtu yeyote hata asipokuwa mbunge,
kwa kweli sijui na sifikirii kama watakuwa wamefikia huko,”alisema
Ndugai.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alithibitisha kumpigia simu Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari
kumpa wito wa kufika mbele ya kamati hiyo ya Bunge na pia alimwagiza
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karatu (OCD), kuwapa taarifa Mbunge wa Karatu,
Israel Natse na Mbunge wa Viti Maalumu Cecilia Paresso.
SOURCE::MTANZANIA