Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa
MWANANCHI
Polisi
Zanzibar imesambaza picha ya mchoro ya mtu anayedaiwa kumuua kwa kumpiga
risasi, Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki mwezi uliopita. Mchoro
huo uliosambazwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisi ya Kamishna wa
Polisi Zanzibar, unamwonyesha mtu aliyevaa kofia ya baraghashia. Katika
taarifa hiyo, Polisi ilisema kwamba mtu atakayesaidia kukamatwa kwa
mtuhumiwa huyo atazawadiwa Sh10 milioni... “Mwananchi yeyote ambaye
anamjua mtu aliyefanana na mchoro huo atoe taarifa katika kituo chochote
cha polisi na iwapo atakuwa ndiye mhusika
atapewa
zawadi hiyo.”
Kamishna wa
Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa hakupatikana jana kutoa maelezo zaidi
juu ya hatua hiyo, lakini Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini
Magharibi, Haji Abdallah Hanna alithibitisha kuwa taarifa hiyo imetoka
Polisi.
Hata hivyo,
Kamanda Hanna hakuwa tayari kutoa ufafanuzi zaidi kwa maelezo kwamba
upelelezi wa suala hilo unafanywa na Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Kuuawa kwa
Padri Mushi lilikuwa tukio la tatu kubwa la kushambuliwa kwa viongozi wa
dini baada ya kumwagiwa tindikali kwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar,
Fadhil Soraga na kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki.
Kitendo cha kutoa picha hiyo ni hatua kubwa katika upelelezi wa kifo cha
Padri Mushi, ambacho kilitikisa visiwani Zanzibar.
Pia hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kutua kwa maofisa wa Shirika
la Upelelezi la Marekani (FBI), ambao wanasaidiana na Polisi wa
Tanzania kuchunguza tukio hilo.
FBI wana
kawaida ya kutumia picha na michoro pale wanapochunguza matukio makubwa
ya uhalifu au ugaidi.
Mathalan,
pale wanapotaka kupeleleza kwa kutumia michoro ya sura za wahalifu
wasiowafahamu, hufanya mahojiano na watu waliokuwapo kwenye tukio na
wakati wakipata maelezo hayo, huwa na wataalamu wao wa uchoraji karibu
ili kujaribu kutengeneza sura za watu wanaotafutwa.
FBI
walikuja nchini baada ya kualikwa na Serikali ya Tanzania ambayo inataka
kujua chanzo cha vitendo vinavyotishia maisha ya viongozi wa dini huko
Zanzibar.
Hii ni mara
ya pili kwa FBI kufanya kazi Tanzania baada ya mwaka 1998 walipokuja
kuchunguza kulipuliwa kwa bomu kwa ubalozi wa Marekani.
No comments:
Post a Comment