Kamati za Kudumu za
Bunge zinatarajiwa kuanza kukutana na kutekeleza majukumu ya Kibunge
jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 18, ikiwa ni kipindi cha nusu muhula
wa uhai wa Bunge.
Vikao vya kamati hizo vitaanza mara
baada ya kukamilika kwa uundwaji wa Kamati Mpya za Bunge pamoja na
uchaguzi wa wenyeviti wa Kamati hizo utakaofanyika Ijumaa ya wiki hii.
Mwishoni mwa
mkutano wa 10 wa Bunge mwezi uliopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda
alitangaza mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe.
Kutokana na
mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC) ambayo itaendelea na jukumu lake la msingi la kuchambua
taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pia kwa
Serikali Kuu.
Kamati nyingine
iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo, huku zikiundwa kamati mpya tatu na
kuzifanyia marekebisho nyingine ikiwa ni hatua ya kuimarisha usimamizi
wa Bunge kwa shughuli za Serikali.
Katika mchakati huo,
kamati mpya zilizoundwa ni Kamati ya Bajeti, Kamati ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo
imetenganishwa kutoka katika Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Kwa mujibu wa Spika Makinda, majukumu ya kamati mpya ya
bajeti ni kufuatilia utekelezaji wa bajeti ya Serikali na sera za fedha
pamoja na kuainisha na kupendekeza vyanzo vya mapato ya Serikali na
kufuatilia mwenendo wa uchumi.
Kamati hiyo ya bajeti pia imepewa jukumu
la kushauri kamati nyingine zote kuhusu bajeti.
Taarifa iliyotolewa
jana na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ya
Ofisi ya Bunge iliyolenga kuufahamisha umma juu ya kuanza kwa kamati
hizo nyeti za Bunge.
“Baada ya uundwaji
wa kamati mpya na uchaguzi wa wenyeviti, litafuatia zoezi la wajumbe
wapya wa Kamati hizo kuhudhuria semina maalumu kuhusu majukumu ya Kamati
pamoja na kupitia mpango wa kazi (work plan)” ilisema sehemu ya taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo ilisema ratiba iliyopo inaonyesha kuwa kamati
za kisekta zitatembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyokasimiwa na
utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2012/13 kuanzia Machi 18 hadi
Machi 23 mwaka huu.
“Tarehe 25 mwezi
huu, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitoa muhtasari kwa wabunge wote
kuhusu mkutano wa 11 wa Bunge ikifuatiwa na kupokea Mpango wa Maendeleo
kwa mwaka 2013/14 kutoka serikalini pamoja na mwongozo wa matazamio na
upeo wa Bajeti ya 2013/14,” iliongeza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema kuanzia Machi 26
hadi Aprili 5, Kamati za kisekta zitafikiria na kuchambua maombi mapya
ya fedha kwa Bajeti ya Wizara zilizo chini yake kwa mwaka wa fedha
2013/14 ikifuatiwa na Serikali kufanya majumuisho kwa kuzingatia ushauri
wa kamati za kisekta.
Iliongeza taarifa
hiyo kuwa baada ya shughuli hizo za kamati, Mkutano wa 11 wa Bunge ambao
ni Mkutano wa Bajeti utaanza mjini Dodoma Aprili 9.
“Mzunguko wa Bajeti
unakusudiwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Juni, 2013 ili kuipa Serikali
muda wa kutosha kutekeleza majukumu yake,” ilibainisha taarifa hiyo.
Kutokana na
mabadiliko hayo, taarifa hiyo iliwataka wabunge kufika Dar es Salaam
keshokutwa ili kuanza shughuli za kamati mapema kama zilivyopangwa
katika ratiba mpya.
No comments:
Post a Comment