Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Michael Hafidh (kulia) akifurahia jambo na Fred Msongole.
MAASKOFU wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini, wamepongeza
uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwajibisha watendaji wake, huku wakimtaka
asiishie kuchukua hatua kwa waliotajwa kuhusika na sakata la Akaunti ya
Tegeta Escrow pekee, bali pia wazembe na wote wanaokutwa na tuhuma
mbalimbali katika utawala wake.
Aidha, wamesisitiza kamwe asicheke nao, kwani kitendo cha kuwavumilia
kinaweza kugeuka shubiri katika utawala wake kwa kuwa watamharibia
kazi. Walisema hayo kwa nyakati tofauti katika salamu zao za maadhimisho
ya Sikukuu ya Krismasi, jana.
Weka pembeni Akiongoza mahubiri katika Ibada Kuu ya Krismasi katika
Kanisa la Champlesy la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Askofu Michael
Hafidh wa Zanzibar, alishauri Rais Kikwete aendeleze utaratibu wa
kuwawajibisha viongozi wazembe na wasio waadilifu katika kazi zao.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
Alisema: “Rais Kikwete, viongozi wazembe na wenye kashfa usiwachekee
kabisa, watakuangusha. Ukiona kiongozi anazembea weka pembeni tu, kuwa
kama kocha, ukiona mchezaji hachezi vizuri weka pembeni, chagua
mwingine, watu wanataka nchi iwe na amani na maisha bora kwa Watanzania
wote.
“Hakuna sababu ya kumuonea aibu mtu, endelea hivyo hivyo, mtu
akikosea unamwambia akae pembeni unachagua mwingine, shida yetu ni
ushindi nchi yetu iwe na amani.”
Alisema viongozi wanapopata nafasi ya kuongoza haimaanishi wao
wanajua zaidi, ila wamepewa neema kuongoza na kwamba Watanzania wana
hazina ya wasomi, hivyo wasilewe madaraka na badala yake waifanye kazi
waliyoaminiwa kuifanya kwa niaba ya Watanzania.
Alisema anashangazwa kusikia kiongozi katika jamii anakuja na ahadi
kemkem, zikiwamo za kuwapelekea wananchi huduma za maji, umeme,
barabara, dawa hospitali, ilhali zote ni haki za msingi za mpigakura.
“Ifike mahali watu watafute njia nyingine za kutafuta kura, si sera
zile zile za maji, umeme, madawa, barabara nzuri…kwanini uende kwa
mwananchi kumshawishi kumpa haki yake ya msingi? Wewe tafuta njia bora
ya kuisaidia jamii unayoiongoza, si kugeuka mzigo kwa Mtanzania,”
alisema na kuongeza kuwa, kwa kushindwa kutimiza majukumu yao, viongozi
wa aina hiyo husababisha chuki dhidi ya serikali na kukata tamaa, hali
inayoweza kusababisha kuvunjika kwa amani.
Viongozi wa dini kugeukia siasa Aliwataka viongozi wa dini na
kuwataka kuachana na siasa, kwani jukumu lao ni kuombea taifa na
viongozi wake sio kuingia katika migogoro ya wanasiasa na kuanza
kuhubiri siasa katika nyumba za ibada.
“Tunataka kusikiliza habari njema kanisani, sasa viongozi wa dini
wakisimama majukwaani ni kubomoana tu, wakisikia jambo bungeni nao
wanalidaka, kazi yetu ni kupiga goti kuwaombea sio kuungana nao,”
alisema Askofu Hafidhi.
Askofu huyo aliwataka pia wanahabari kuzingatia maadili ya uandishi
katika kutoa taarifa kwa jamii kwa sababu habari nyingine zinasababisha
chuki kwa wananchi, hivyo wasiangalie mauzo ya kazi zao pekee, bali pia
wageukie uzalendo kwa nchi yao.
Akitoa salamu za Krismasi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Dk Alex Malasusa, Askofu Hafidhi alisema
nchi inakabiliwa na mambo makuu ambayo ni Uchaguzi Mkuu pamoja na ule wa
kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa, hivyo wananchi wanatakiwa kuwa
makini kuepuka vurugu za aina yoyote.
Alisema amani imedumu kwa miaka mingi, ingawa zilijitokeza vurugu
kidogo katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni,
hivyo badala ya kuichezea, ni vyema ikatunzwa mithili ya mboni ya jicho.
JK asiishie Escrow Mawazo ya Askofu Hafidhi yameshabihiana na yale ya
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Dodoma, Amon Kinyunyu aliyeitaka serikali isiishie kuwaadhibu wachache
waliotajwa kwenye sakata la Escrow, bali ihakikishe wote waliohusika
kwenye tuhuma hizo, wanachukuliwa hatua za kisheria na wanarudisha fedha
walizoiba ili kuleta amani.
Alisema pamoja na baadhi ya waliotajwa katika sakata la Escrow,
kuondolewa katika nyadhifa walizokuwa nazo wanatakiwa kurudisha fedha
walizoiba na kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa viongozi
wengine wa umma.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa mahojiano mara baada ya kumalizika
kwa ibada ya Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kilutheri mjini
hapa. Alisema sasa nchi inatakiwa kuomba ili iweze kupata viongozi
wenye hofu ya Mungu wenye moyo wa kutumikia wananchi ;na si tu kujali
maslahi yao binafsi huku kundi kubwa la wananchi wakiishi kwenye
umasikini.
Pia, aliitaka Serikali kuchukua hatua za haraka katika kuwawajibisha
mafisadi ili kukomesha vitendo hivyo, ambavyo vimekuwa vikiita hasara
nchi. Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
“Hatua ziwe zinachukuliwa mapema isiwe mpaka wananchi wanaanza kupiga
kelele na kuhatarisha usalama wa nchi,’ alisema. Askofu Kinyunyu
alisema tatizo kubwa lililopo jambo linapotokea linachelewa kuchukuliwa
hatua mpaka wananchi wapige kelele na ndipo maamuzi yafanyike.
Alisema hata maamuzi mengi yanakuwa ya zimamoto, lakini kinachotakiwa
ni kutekeleza na kusimamia maadili na hata sheria za utumishi wa umma.
Askofu kinyunyu alisema tatizo kubwa kwa baadhi ya Viongozi wanapoingia
madarakani wanawaza kujilimbikizia mali wao hawakumbuki kuwahudumia
wananchi wengine.
Alisema hali hiyo imekuwa ikichangia wananchi kukosa huduma muhimu.
“Serikali isiishie kuwaadhibu hao wachache wanaotajwa kwenye sakata la
Escow, bali ihakikishe wote waliohusika kwenye tuhuma hizo,
wanachukuliwa hatua za kisheria ili kuleta amani,” alisema.
Pia, aliitaka Idara ya Maadili ya Utumishi wa Umma kufanya kazi zake
bila kumwonea mtu yeyote ili wote waliohusika wafikishwe kwenye vyombo
vya sheria na sheria ifuate mkondo wake. Awali, akihubiri katika ibada
ya Krismasi aliwataka watu wote kudumisha amani na upendo.
Alisema maana ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni amani na upendo hivyo
watu washerehekee kwa kukumbuka kudumisha mambo hayo. “Maana ya Krismasi
ni amani na upendo ni lazima tuhakikishe tunadumisha mambo hayo ambayo
ni muhimu sana katika maisha.
Fagio la chuma Askofu Dk Martin Shao wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini,
amesema fagio la chuma alilokabidhiwa Rais Jakaya Kikwete na Watanzania,
amekuwa akilitumia vizuri katika kufagia uozo wote unaofanyika.
Alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu maalumu ya Krismasi kwa
taifa, kwa niaba ya Dayosisi ya Kaskazini. Alisema Rais Kikwete amekuwa
akitumia busara na hekima kubwa katika kufanya maamuzi makubwa ya nchi.
Alisema amekuwa akitumia fagio lake la chuma vizuri katika kuondoa
uchafu, unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu. Mbali na
kumpongeza Rais Kikwete kwa hotuba yake nzuri ya hivi karibuni, alisifu
pia uamuzi wa kutengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, lakini pia askofu huyo akaongeza kuwa,
bado Watanzania wanasubiri amalizie kazi iliyobaki.
Alisema Watanzania wameridhika na maamuzi ya Rais kuhusu sakata la
akaunti ya Tegeta Escrow, na kueleza kiu kubwa wanasubiri kuona maamuzi
makubwa yatafanyika zaidi ya hayo.
Alimtaka Rais Kikwete kuendelea kuwa na ujasiri wa hali ya juu, wa
kutumia fagio lake la chuma, kwa kufagia watu wote wanafanya ubadhirifu
wa mali za umma, na watumishi wote wanaokiuka maadili ya utumishi na
kujilimbikizia mali.
“Rais wetu ameweza kutumia vizuri fagio lake la chuma katika kufanya
maamuzi, nampongeza sana kwa hotuba yake iliyojaa busara na maamuzi
mazuri, lakini atambue Watanzania bado wanasubiri maamuzi mengine
yaliyobaki kiporo kwa hamu kubwa….tunaamini atafanya maamuzi mazuri
zaidi,” alisema Askofu Shao.
Katiba Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa alisema ni vyema
Watanzania wakaisoma Katiba Inayopendekezwa kipengele kimoja kimoja na
kuielewa, ili ukifika wakati wa kuipigia kura waweze kukubali au kukataa
kitu wanachokijua wao wenyewe.
Alisema kila Mtanzania anatakiwa kuitambua Katiba yake ambayo haina
maslahi kwa chama chochote. “Tusiache watu wasome Katiba Inayopendekezwa
kwa ajili yetu, au kutusemea yaliyomo, ni vyema kila Mtanzania akaisoma
na kuielewa ili wakati wa kuipigia kura afanye maamuzi akiwa
anaitambua,” alisema Askofu Shao.
Uchaguzi mkuu ujao Katika uchaguzi mkuu wa mwakani, Askofu Shao
amewataka Watanzania kuliombea taifa, kwani ndicho kipindi cha kuitafuta
amani bila ya kujali itikadi za kidini na siasa.
Aliwataka Watanzania kutokubali kununuliwa wa baadhi ya wagombea
katika nafasi za udiwani, wabunge na urais watakaohitaji madaraka, kwa
lengo la kuwapigia kura, na badala yake waangalie kiongozi mwadilifu.
Askofu Shao alisema taifa linahitaji kiongozi mwenye hofu ya Mungu,
bila kuangalia chama cha siasa, ambaye atakuwa mwadilifu katika kutunza
na kulinda rasilimali za Watanzania, pamoja na amani iliyopo.
Asante kwa kutembelea blog hii ya Jambo Tz,
ili kuboresha blog yetu tunatoa fulsa ya kutangaza matangazo mbalimbali
na pia kutoa maoni yako kupitia namba ya simu (WhatsApp & SMS) 0715
221198, E-mail jambotz8@gmail.com. Merry Chistmass & Happy New Year.
No comments:
Post a Comment