Waziri wa Maji, Prof Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari
wa gazeti hili, walipomfanyia mahojiano maalumu ofisini kwake mjini
Dodoma, hivi karibuni.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe
ameshangazwa na utitiri wa watu wanaotaka kugombea urais kwenye
Uchaguzi Mkuu 2015, akisema nafasi hiyo ya juu nchini haifanani na
mashindano ya urembo ambayo mtu yeyote anaweza kujaribu.
Mbunge huyo wa Mwanga alisema watu hao
wanaojitokeza kuwania urais hawaelezi wanataka kulifanyia nini Taifa na
akashauri wasioweza kueleza hoja zao wasichaguliwe kushika nafasi hiyo.
“Urais unahitaji kuwa na sifa, dira na ajenda kwa
Taifa,” alisema Profesa Maghembe wakati wa mahojiano maalumu na gazeti
hili mjini hapa.
Kauli ya Profesa Maghembe imekuja wakati Taifa
likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2015, huku chama
chake, CCM kikikabiliwa na kazi ngumu ya kumpata mrithi wa Rais Jakaya
Kikwete ambaye anamaliza muda wake. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Hali kama hiyo iliikumba CCM wakati wa uchaguzi wa
kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 wakati takriban watu 20 walipojitokeza
kutaka kuingia Ikulu na baadaye mwaka 2005 wakati wa uchaguzi
uliomuweka madarakani Rais Kikwete.
Ndani ya CCM, mjadala huo sasa umekumbwa na hoja
ya umri baada ya makada vijana kujitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais
Kikwete kupambana na wanasiasa wakongwe, baadhi wakiwa ni wale
waliojiandaa kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Profesa Maghembe alipuuza mjadala huo
wa umri wa mtu kugombea urais akisema kuwa hauna msingi na kwamba sifa
kuu ya mgombea urais ni ajenda ya kuliletea Taifa maendeleo endelevu.
“Umri hauwezi kuleta tofauti katika uongozi wa
nchi. Ni kama kusema jiwe liwe rais,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe,
ambaye amefanya kazi wizara tofauti tangu Januari 2006 aliposhika
uwaziri kwa mara ya kwanza.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka mgombea urais awe na umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea.
“Hivyo haisemi kuwa ukishakuwa na miaka 70 huwezi
kuwa rais ama haisemi ukiwa na miaka 40 unafaa zaidi kuwa rais.
Inategemea huyo mtu anayegombea anataka kuwafanyia nini Watanzania,”
alisema.
Waziri huyo wa saba tangu Wizara ya Maji
ianzishwe, alisema kugombea urais kunategemea ajenda aliyonayo mtu na
hata watu wanapokwenda kumchagua, lazima waangalie ana ajenda gani.
“Ikulu si mahali pa kukimbilia, mimi hata sijui wanakimbilia nini kwa
sababu lazima mtu uwe na ajenda. Na kama mnasikia mtu anasema mimi
nataka kuwa tu rais, huyo hafai kabisa,” alisema.
“Lazima mtu anayetaka kuwa rais atueleze uchumi
sasa unakua kwa asilimia saba na umekuwa hivi kwa karibu miaka 10 lakini
ni jambo linalofanya umaskini uwe mkali kabisa na usiishe ni kutokana
na shughuli inayofanywa na watu wengi ya kilimo, kuwapatia kipato haikui
kama sekta nyingine.
Alitoa mfano sekta ya usafirishaji ambayo inakua kwa zaidi ya
asilimia 28 na sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 18, lakini sekta ya
kilimo inakuwa kwa asilimia 4.2 tu wakati ndiyo inabeba karibu asilimia
77 ya Watanzania.
“Lazima hali hii ibadilike huko tunakokwenda. Sasa
huyu rais atuambie ataibadilishaje. Mtu anasema anataka aende Ikulu
akae hata saa moja tu, sasa saa moja unafanya nini? Hata nusu saa wewe
unataka kwenda hapo kufanya nini?” alihoji. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Alisema kwa kipindi hiki ni lazima mtu anayetaka
urais awaeleze Watanzania atawezaje kuivusha nchi katika uchumi wa kati,
vinginevyo haifai kushika nafasi hiyo.
“Naona watu wengi wanatangaza, mimi nataka kuwa
rais, mimi nataka kuwa rais. Ehhh unatakuwa rais (anaitika ehh),
Watanzania unawaondoaje hawa asilimia 77 waungane na wengine ili baada
ya miaka yako 10 tuwe katika uchumi wa kati?” alisema.
Alisisitiza mtu ambaye anataka kuwa rais lazima
awe na sifa na ajenda. “Lazima atueleze ajenda yake nini? Siyo kwamba si
unaniona mimi hata wakipiga picha nafaa kuwa rais, hata kidogo,”
alisema na kuongeza;
“Urais siyo kama mashindano ya Lundenga ya
kupeleka warembo kwenda kuwashindanisha hata kidogo. Is Very important
(ni muhimu sana), mimi nadhani ndiyo sifa ya msingi.”
Wanawake na urais
Profesa Maghembe alisema haamini kwamba wanawake
bado hawawezi kushika nafasi hiyo ya juu serikalini. Wapewe fursa
washindwe wenyewe.
Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, wanawake wenye sifa ya kuwania urais na kushinda wapo na wakiweza wajitokeza ili wapigiwe kura.
“Unajua kuna wengine wanasema ni mapema. Lakini
tangu lini saa hizi saa nane mchana unasema ni mapema, unataka wangoje
usiku! Wamama wapo lakini na muda wa kutangaza nia bado upo,” alisema na
kuongea:
“Pia tunaangalia hawa waliotangaza nia wataifanyia
nini Tanzania. Kama wako ambao wanaweza kufanya hiyo kazi, mnaingia
huko, siyo marathon.”
Kuhusu ubunge wake
Profesa Maghembe alisema kuwa kazi yake ya ubunge anaipenda sana
na kwamba ni kazi inayohitaji nguvu, ubunifu na kuwa tayari kukabiliana
na changamoto za maendeleo.
“Na ni kazi ambayo inahitaji nguvu, ubunifu na
inahitaji kuwa tayari kukabiliana na changamoto za maendeleo. Kazi hiyo
naipenda sana na bado nina nguvu na nia ya kuifanya. Kwa hiyo katika
uchaguzi mkuu ujao nitagombea katika jimbo langu la Mwanga.
“Kwa hiyo mimi siwezi kusema kuwa nikipata
upinzani ni kitu kama unfair (siyo cha haki) hivi, hata kidogo. Ni kitu
ambacho ni sehemu ndani ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Profesa Maghembe alisema ushindani ni kitu ambacho anafahamu kitakuwapo.
“Kila wakati ushindani unakuwa mkubwa zaidi,
nimepita katika chaguzi tatu na kila wakati upinzani unakuwa mkali
zaidi. Nategemea katika mwaka 2015 ushindani utakuwa ni mkubwa zaidi
lakini nategemea nitashinda kwa kishindo zaidi,” alisema.
Alisema hakuna kosa kwa watu kushindana katika chaguzi na ni haki yao ya uanachama.
Alipoulizwa mambo matatu yanayomfanya kutegemea
kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao, Profesa Maghembe alisema
mojawapo ni utekelezaji wa ilani ya CCM na miradi ya maendeleo
imetekelezwa.
“Wananchi matatizo yao yametatuliwa kwa kiwango
kikubwa sana na tupo karibu nao, kuwasikiliza na kuona kuwa tunaelekea
wapi,” alisema. Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Alisema pia wananchi huangalia historia ya kipindi
ambacho umeongoza na katika jimbo lako wamekuwa wakipiga hatua kila
kipindi na kutokana na hayo utashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu
ujao.
Nafasi ya upinzani
Profesa Maghembe alisema “Njaa ya wananchi wengi
ni maendeleo, hivyo kile chama kinachowaahidi Watanzania kuwaletea
maendeleo kitaendelea kushinda wakati wote,” alisema na kuongeza:
“Kile kinacholeta matumaini ya mkate wao wa kila
siku, kuwapatia watoto shule kuendeleza vyuo vikuu, huduma nzuri za
afya, maji na kuhakikisha mazao kuingia sokoni ili wapate bei nzuri
kitaendelea kutawala Tanzania kwa muda mrefu.”
Alisema bado vyama vingi nchini vinaona kuwa kusimama majukwaani, kutoa sauti kubwa na ukali mwingi ndiyo kutawala nchi.
Alisema vyama vitakapofika kwa wananchi katika
ngazi ya chini na kutoa mpango mbadala ya kuleta maendeleo nchini ndiyo
vitaweza kuwa na ushindani. Alisema hivi sasa vyama vya upinzani havina
ushindani na CCM. “Wakina Sangara, operesheni delete, kudelete
haiboreshi shule,” alisema.
Katiba
Katika hatua nyingine, Profesa Maghembe
alibainisha kuwa Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaendelea vizuri, ila
kinacholeta mgogoro ni kitendo cha Tanzania kuingia kwenye mchakato huo
wakati bado Katika yake ya mwaka 1977 haijapoteza sifa.
Amesema Katiba hiyo iliyotuongoza kwa miaka 50 iliyopita bado ni nzuri, ndiyo maana kuna maoni tofauti juu ya mchakato wenyewe.
Alisema Katiba iliyopo imewatumikia vizuri lakini
wakasema kuna fursa nzuri ya kutengeneza Katiba nzuri zaidi ya
kuwatumikia vizuri zaidi kwa miaka zaidi ya 100.
“Watanzania tumekuwa kama wale watu ambao wana koti halijachakaa, zuri tu lakini wakapeleka kwa fundi liwekwe kiraka,” alisema.
“Hapo ndiyo tatizo, kwa sababu katika nchi, Katiba
ni matokeo ya vita, wamepigana vita sasa wamechoka wanataka tuongee
amani, tunaandika Katiba,” alisema na kuongeza:
“Sasa sisi tunaandika Katiba mpya tukiwa na amani.
Hatuna tatizo kubwa kwamba watu wanapoongalia changamoto hawaliongelei
hilo kama tatizo kwa sababu tunayo Katiba nzuri ambayo imetubeba kwa
miaka 50.” Asante
kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza
kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya
neno Jambo Tz
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment