Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) jana Aprili 28, 2018 amemtembelea msanii nguli wa filamu Bw. Amri Athumani (Mzee Majuto) ambaye alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Tumaini, Dar es Salaam.
Dkt. Mwakyembe akizungumza katika tukio hilo amesema Serikali imeamua kumpeleka Mzee Majuto nchini India kwa ajili kupata matibabu zaidi.
"Kwa kuanzia tumeamua kumuhamishia Mzee Majuto katika hospitali ya Muhimbili ili kukamilisha maandalizi muhimu ya kiafya kabla ya safari ya kuelekea India", alisema Dkt. Mwakyembe.
Waziri Mwakyembe alisema matibabu atakayopata Mzee Majuto akiwa katika hospitali Muhimbili na akiwa nchini India yatagharamiwa na Serikali.
Wakati huo huo kampuni zilizowahi kufanya kazi na Mzee Majuto zimeitikia wito wa kumchangia ambapo kampuni ya Azam Marine imetoa fedha sh. Milioni 5, Azam Media Sh. Milioni 5, kampuni ya Ivory Chocolates Shs. Milioni 10 na tiketi moja ya ndege, na kampuni ya ASAS imetoa tiketi 2 za ndege.
Dkt. Mwakyembe amewakumbusha wadau mbalimbali kuendelea kumchangia Mzee Majuto ili kuwezesha familia yake kujikimu katika kipindi hiki ambacho Mzee Majuto anapatiwa tiba.
Waziri Mwakyembe akiambata na Mwanasaa Steve Nyerere na Afisa Habari wa Chama cha Wasanii wa Filamu Bw. Kaftany amewataka Wanasaa kuendelea kushirikiana na kusaidiana kwa ukaribu.
No comments:
Post a Comment