Na Fidelis Butahe na Sharon Sauwa, Mwananchi
Kelele, kukunjana na
kunyoosheana vidole jana mchana vilitawala nje ya ukumbi wa Bunge wakati
wabunge wa CUF kutoka Zanzibar walipotaka ‘kumkanya’ Mbunge wa Nkasi
Kaskazini (CCM), Ally Keissy.
Sakata hilo la aina yake lililodumu kwa takriban
dakika 15 lilitokea saa 7:05 mchana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai
kuahirisha kikao cha Bunge.
Wabunge hao Mussa Haji Kombo (Chakechake), Kombo
Khamis Kombo (Magogoni) na Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe),
walitaka ‘kumkanya’ Keissy kutokana na kile alichosema alipokuwa
akichangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
mwaka 2014/15 na kusema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina
haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.
Kauli hiyo licha ya kulalamikiwa na wabunge wote
wa CUF kutoka Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kusimama na kuomba
mwongozo wa Spika, Keissy alizidi kuwashambulia na kusema kuwa majimbo
ya Zanzibar watu wake wanaweza kukusanywa sehemu moja kwa kupigiwa
filimbi tu.
“Nyie Zanzibar idadi yenu ya watu ni asilimia 2.8
ya watu wote wa Tanzania. Sasa mnataka kupata kila kitu sawa ili iweje!
Mnataka ajira asilimia 21 na Watanganyika wakafanye kazi wapi?” alisema
Keissy.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho na wabunge
kuanza kutoka nje, wabunge hao wa CUF walikwenda kumsubiri Keissy karibu
na jengo la kantini. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Mbunge wa kwanza kumvaa Keissy alikuwa Khamis
Kombo ambaye kabla ya kumfikia alizuiwa na Mbunge wa Mpanda Kaskazini
(CCM), Moshi Selemani Kakoso.
Wakati Keissy akishangaa alitokea Haji Kombo ambaye naye alizuiwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Abdulsalaam Selemani Amer.
“Mimi sitaki kupigana bwana ninachokijua ni kwamba
nilikuwa nikichangia mjadala wa bajeti na nilichokisema ni ukweli
mtupu,” alisema Keissy huku akiwa amenyanyua mikono yake juu na kuondoka
eneo hilo.
“Wewe (Keissy) sijui una nini wewe. Unapenda
kutufuata fuata sana watu wa Zanzibar. Hivi una nini wewe? Hivi hujui
kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar?”
alisikika akisema Khamis Kombo.
Kwa upande wake, Sanya hata baada ya wenzake
kutawanyika eneo hilo, aliendelea kumlaumu Keissy na kuwataka wabunge wa
CCM kumuonya.
“Anapenda sana kutoa kauli mbaya dhidi ya
Zanzibar. Jamani mkanyeni mwenzenu haiwezekani kila siku awe yeye tu
anayetukashifu bungeni,” alisema Sanya huku akitulizwa na mbunge wa
Kibiti (CCM), Abdul Jabiri Marombwa.
Baadaye Keissy alisema: “Nimesema ukweli kabisa hakuna jambo
hata moja la uongo. Sina kosa hata kidogo kwa sababu nimeonyesha ujasiri
kwa kusema ukweli.”
Kwa upande wake, Haji Kombo alisema: “Ana kauli za
kibaguzi sana na tulitaka kumkanya tu na siyo kumpiga.” Alisema mbunge
huyo amekuwa akitoa kauli za kibaguzi na kwamba walimvamia kutokana na
kupandwa na jazba.
“Ndiyo maana siku zote tunasema Muungano wa
Serikali mbili siyo muungano kabisa, ni bora Serikali tatu,
alichokifanya si kitu kizuri.”
Sakata lilivyoanza
Sakata hilo lilianza wakati Haji Kombo akichangia
bajeti ya Mambo ya Nje na kueleza kuwa Zanzibar haitendewi haki katika
uteuzi wa mabalozi nje ya nchi, akisema haiwezekani iwe na asilimia 1.3
ya mabalozi 34 wa Tanzania.
“Bajeti hii ipo katika mambo ya Muungano lakini
Zanzibar ina mabalozi wanne tu, huku ni sawa na kuoneana. Tanganyika
inaifanya Zanzibar kama koloni lake. Ndiyo maana tunasema Tanganyika
imevaa koti la Muungano,” alisema Kombo. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Ilipofika zamu ya Keissy kuchangia mjadala huo
alisema: “Idadi ya Wazanzibari ni asilimia 2.8 ya Watanzania wote na
wala hamchangii gharama ya Muungano kwa miaka 20 sasa. Hao mabalozi
wanalipwa kwa kodi za wananchi wa Nkasi, Biharamulo na Dar es Salaam.”
Keissy alimtaka Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard
Membe atakapokuwa akijibu hoja za wabunge aeleze, Zanzibar inachangia
kiasi gani katika Muungano.
“Mnasema upande mmoja umevaa koti la Muungano,
hata sisi (Tanganyika) koti hilo limeshaanza kutubana. Kama koti
limewavaa amueni moja njia mbona nyeupe, acheni chokochoko zenu,”
alisema Keissy na kuongeza:
“Fedha za mfuko wa jimbo mnachukua mara mbili
(kwenu na Bara). Kwanza jimbo moja la Zanzibar ni kama mawili ya jimbo
la Nkasi na hata ukitaka kuwaita watu wake unapiga filimbi tu wote
wanakusanyika.”
Keissy alizidi kuwapandisha hasira wabunge hao baada ya kuwaeleza kuwa Zanzibar hailipi umeme unaotoka Bara.
“Usimchokoze mwehu halafu unakimbilia nyumba ya
vioo. Sisi pia tuna uchungu na nchi yetu, hatuna maji wakati kwenu
mnasema kila mtu anapata maji na umeme.”
Baada ya kauli hiyo Haji Kombo aliomba mwongozo kwa Spika na
kabla ya kupewa ruhusa, Keissy alisikika akisema, “Toa taarifa
nitakujibu.”
Katika mwongozo wake Kombo alisema, “Nchi hii haina wendawazimu namna hii. Hii ni nchi yenye heshima na watu wanaoheshimiana.”
Kauli hiyo ilimchefua Ndugai ambaye alimkatisha
Kombo na kumtaka aeleze mwendawazimu ni nani. “Mwendawazimu ni mtu
anayesema maneno yasiyo na busara. Wazanzibari siyo watu maskini na
wameingia katika Muungano kwa masikitiko makubwa. Kati ya Watanzania
milioni 45, Wazanzibari wapo milioni 1.3 tu,” alisema Kombo na kuongeza:
“Hakuna chochote mnachotusaidia. Ni aibu mbunge wa
CCM, chama ambacho kimekubali kuungana na Zanzibar kuzungumza maneno
kama haya. Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika, mwambie (Kessy)
asivuke kuja Zanzibar.”
Hata hivyo, Ndugai aliukataa mwongozo huo kwa
maelezo kuwa ulikuwa ni taarifa tu na kumtaka Keissy kujibu taarifa
hiyo. “Siikubali hiyo taarifa na namwona yeye ndiyo mwendawazimu zaidi.”
Kessy alisema lazima Zanzibar ichangie Muungano
kama inataka kuwa na idadi sawa ya mabalozi kauli ambayo iliwafanya
wabunge wa CUF kutoka Zanzibar kusimama, huku Mbunge wa Ole, Rajab
Mbarouk Mohamed akiomba mwongozo.
“Jamani niacheni nizungumze mbona nyinyi
mlizungumza na mkaachwa. Subirini nimalize kuchangia mwiba unatokea
ulipoingilia, vumilieni tu na kama hamtaki tokeni nje,” alisema Keissy.
Ndugai aliingilia kati na kusema, “Naona mmeamua
kuleta mada ya Bunge Maalumu la Katiba la Mheshimiwa Sitta (Samwel).
Subirini litakapoanza.” Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment