Pretoria, Afrika Kusini. Rais Jacob
Zuma amezindua sanamu ya shaba ya shujaa wa Afrika, Nelson Mandela
kwenye jengo la Muungano lililopo mji wa Pretoria.
Sanamu hiyo yenye urefu wa mita tisa humuonyesha Mandela akitabasamu, huku akiwa ameonyesha ishara ya kukumbatia.
Wakati akizindua sanamu hiyo jana,
Rais Zuma alisema kwamba sanamu nyingi za Mandela zinamuonyesha
akinyoosha mkono wake mmoja juu kama ishara ya mapambano iliyokuwa
ikitumiwa na Chama cha ANC.
Lakini, ishara ya kukumbatia iliyokuwa
ikitumika katika sanamu hii ni tofauti, kwasababu inamuonyesha Madiba
akikumbatia nchi nzima na watu wake wote bila kujali rangi, itikadi wala
tabaka. Zuma aliizindua sanamu hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa
mazishi ya kiongozi huyo yaliyoshuhudiwa na umati mkubwa watu
mbalimbali, wakiwamo viongozi wa nchi tofauti yaliyofanyika katika
Kijiji cha Qunu.
Katika uzinduzi huo alikuwapo Waziri
wa Utamaduni, Paul Mashatile na familia ya Madiba ambapo Zuma alikuwa na
mkewe, Thobeka Madiba Zuma.
Pia, alikuwapo Makamu wa Rais, Kgalema
Motlanthe na viongozi wengine nchini humo wakishuhudia kuzinduliwa kwa
sanamu hiyo ya historia. Uzinduzi huo uliofanyika katika jengo hilo, pia ulishuhudiwa na waandishi wa habari kutoka sehemu mbalimbali.
Mandela alizikwa juzi katika kijiji
ambacho alizaliwa cha Qunu, mazishi yake yalihudhuriwa na umati mkubwa
wa watu wakiwamo viongozi mbalimbali duniani.
Na Mwandishi wetu, Mwananchi
No comments:
Post a Comment