TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Asikitishwa na idadi kubwa ya wasafirishaji wa dawa za kulevya
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewasili Beijing, China saa 10 leo jioni (Jumatano,
Oktoba 16, 2013) na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi
yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.
Mara
baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Beijing, Waziri Mkuu
alielekea kwenye nyumba ya wageni ya Serikali ya Diaoyatui ambako
alipokea taarifa fupi kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini China.
Akiwasilisha
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Balozi wa Tanzania nchini China,
Luteni Jenerali (Mst.), Abdulrahman Shimbo alisema sehemu kubwa ya
utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania na China iko chini ya mwamvuli wa
FOCAC (Forum on Africa China Cooperation) ambayo inagawanyika katika
maeneo sita.
Alyataja
maeneo hayo kuwa ni misaada (grants), mikopo ya masharti nafuu
(preferential loans), mikopo ya kibiashara (preferential buyers credit),
uwekezaji, ushirikiano maalum na ushirkianao wa kihistoria.
“Miradi
mahsusi inayogharimiwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na
China imeongezeka sana na inatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni
800 ifikapo mwaka 2014/2015,” alisema Balozi Shimbo.
Kuhusu
elimu na mafunzo, Balozi Shimbo alisema programu hiyo ambayo imeanza
muda mrefu, hadi kufikia Desemba 2011, ilikuwa imekwishawanufaisha
wanafunzi wa Kitanzania 110 na wataalamu 1,020 ambao walipatiwa mafunzo
chini ya udhamini wa Serikali ya China.
Kwa
mwaka huu 2013, Balozi Shimbo alisema kuna wanafunzi zaidi ya 300 ambao
wanasoma nchini humo. “Hivi sasa kuna wanafunzi 31 wanaodhamimiwa na
serikali ya Tanzania, wanafunzi 249 wanaofadhiliwa na serikali ya China
na wengine zaidi ya 100 wanaojidhamini wenyewe katika shahada za Uzamili
na Uzamivu,” alisema.
Pia
alisema Tanzania kwa kushirikiana na Dalian University of China,
itanufaika na mradi wa kupandisha hadhi Chuo cha Usafiri wa Baharini
(Dar es Salaam Maritime Institute) hadi kufikia ngazi ya Chuo Kikuu cha
Kanda ya Afrika Mashariki.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi kwa kampuni ya Kichina ya
China Rail Engineering Group ambayo inakifufua kiwanda cha viatu na
ngozi cha Zanzibar na kukifanya kiwe kiwanda cha samani. Kiwanda hicho
kilijengwa kwa msaada wa Serikali ya China katika miaka ya 70.
Hata
hivyo, Balozi Shimbo alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa
ya kimahusiano na China ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika
magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya
kusafirisha madawa ya kulevya.
“Kati
ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa mashaka. Kati yao 48 wako China
Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10. Kati ya hao 175, wanawake ni
34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China bara,” alisema.
Akizungumza
na maafisa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Waziri Mkuu
alisema tatizo la madawa ya kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja
na mahusiano baina yake na nchi marafiki.
“Tunahitaji
kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za
kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha kusikitisha zaidi ni
idadi kubwa ya wanawake waliokamatwa… wizara zinazohusika inabidi tukae
na kuweka mkakati wa pamoja,” alisema.
Kuhusu
misaada ya China kwa Tanzania, Waziri Mkuu alisema, kuna miradi ya kufa
na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake hii na
kuiainisha kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, usambazaji wa umeme na
ukuzaji wa utalii baina ya Tanzania na China hasa fursa ya kuanzisha
usafiri wa ndege wa moja kwa moja baina ya Chiona na Tanzania.
Kesho
(Alhamisi, Oktoba 17, 2013) Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri
Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China,
Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway
Jianchang Engineering. Pia atahudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa
kwa heshima yake kesho jioni.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 16, 2013
No comments:
Post a Comment