Friday, September 13, 2013

RAIS KIKWETE AONGEZA VIONGOZI WANAOTAKIWA KUTANGAZA MALI ZAO

1_0ddb0.png
Waziri Mkuchika akizungumza kwenye katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari semina hiyo.
2_cd971.png
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda akizungumza na washiriki wa Semina (hawao pichani).Kushoto kwake ni Waziri Mkuchika na Mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti Balozi Jaji Mstaafu Hamisi Msumi.
3_d2313.png
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika akizungumza katika ufunguzi wa Semina.Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti ya Maadili Balozi Jaji Mstaafu Hamisi Msumi na kushoto ni Kamishna wa Sekretarieti Jaji Mstaafu Salome Kaganda.
5_cdb4b.png
Washirikiwa wa Semina wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi wa ufunguzi wa Semina hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika (aliyekaa katika mstari wa mbele).Wa kwanza kushoto waliokaa ni mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani USAID.
Picha zote na Hussein Makame, MAELEZO.

Hussein Makame
RAIS Jakaya Kikwete ameongeza vyeo vya wa viongozi wa umma wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao watapaswa mara moja kujaza fomu za kutangaza mali walizonazo kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari iliyofanyika katika hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam Septemba 12 mwaka huu.
Jaji Mstaafu Kaganda alisema kuwa nyongeza hiyo iliyotiwa sahihi na Rais Kikwete Agosti 14 mwaka huu na tayari na imeshatoka kwenye gazeti la Serikali, inaongeza wigo wa viongozi wa umma wanaotakiwa kutangaza mali zao.
Alitaja vyeo vya viongozi hao walioongezwa kuwa ni Msajili wa Hati, Wasajili Wasaidizi wa Hati wa Kanda, Makamishna Wasaidizi katika Taasisi za Umma, Wakuu wa Hazina ndogo, Wakuu wa Idara na Vitengo na sehemu za ugavi na manunuzi katika Wizara, Idara za Serikali, Wakala wa Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Wengine ni Mtendaji Mkuu Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN),Makanali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Waratibu wa Miradi katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma, Waganga Wakuu wa mikoa, Watendaji Wakuu wa Taasisi, Makatibu, Wakurugenzi na Mameneja katika Taasisi za Umma.
Viongozi wengine walioongezwa ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Wasajili Wasaidizi wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa Kanda, Wenyeviti wa Barza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Polisi wa Wilaya(OCDs), Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya(OCCIDs), Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa(RCOs),Maafisa Usalama wa Wilaya na Mikoa.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika aliwaasa wahariri wa vyombo vya habari na waandishi kwa ujumla kutumia kalamu zenu na midomo yao katika kuheshimu maadili ya kazi zao ili kutoa mchango katika kuijenga Tanzania.
Alisema vyombo vya habari vinayo fursa ya kuishawishi jamii kuendeleza yale mema yaliyo katika jamii, hivyo aliwaomba wanahabari kuhakikisha kwamba wanatumia kalamu zao kuendeleza umoja na amani nchini.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO, Assah Mwambene aliviasa vyombo vya habari kuacha kuwa sehemu ya kuendeleza ajenda za watu badala ya kutekeleza moja ya majukumu yao ya kuweka ajenda zenye muelekeo wa kuijenga jamii ya Watanzania.
Akifafanua juu ya semina hiyo, Waziri Mkuchika alisema semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kujenga uelewa kwa umma kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani USAID.
"Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mdau wakiwemo waandishi wa habarai wanashiriki kikamilifu kuunga mkono jitihada za Serikali kujenga misingi imara ya maadili na utawala bora ili kuongeza kasi ya maendeleo endelevu katika nchi yetu" alisema Waziri Mkuchika
Alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni chombo kilichoundwa kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa dhamana ya kusimamia maadili ya viongozi wa Umma iliyoainishwa katika Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.
Alibainisha kuwa lengo la Sheria hiyo ni kuhakikisha kwamba viongozi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa namna ambayo wanadumisha na kukuza imani na heshima ya wananchi kwa Serikali yao.
Akizungumzia vyeo vya viongozi walioongezwa na Rais Kikwete kutangaza mali zao, Waziri Mkuchika alisema kuwa Sheria imeweka kifungu kinachomruhusu Rais kuongeza idadi ya viongozi wanaotakiwa kutangaza mali zao kila mwaka kwa kadri atakavyoona inafaa kwani hawakuwepo wakati wa kutungwa sheria hiyo.
Mada zilizowasilishwa kwenye semina hiyo ni Umuhimu wa Maadili katika Maendeleo ya Nchi, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Majukumu ya Sekretarieti ya Maadili na Nafasi ya Vyombo vya Habari Katika Kusimamia Maadili na Utawala Bora katika Jamii, ambayo ilikuwa maudhui kuu ya semina hiyo.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...