Kana kwamba
alisikia kilio cha wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa na shauku ya
kumwona lakini ikashindikana, Rais Barack Obama wa Marekani amewaomba
radhi kwa hali hiyo.
Akizungumza
juzi wakati wa dhifa iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wake na
Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Dar es Salaam, Obama alisema
akirudi nchini siku zijazo, atapita mitaani akiwa katika gari la wazi.
"Niliona
wananchi walivyojitokeza kwa wingi kutupokea barabarani, nilifarijika
sana lakini hawakuweza kutuona vizuri kwani tulikuwa ndani ya gari
maalumu-The Beast.
"Miaka ya
sitini Rais John Kennedy alipokuja hapa, alipita na gari la wazi
mitaani wananchi wakamwona, naomba radhi nikija tena nitaonekana,"
alisema Obama.
Watu wengi
waliozungumza na vyombo vya habari walionesha dhahiri kiu ya kutaka
kumwona Rais huyo wa kwanza mweusi wa Marekani, lakini wakaishia kuona
gari lake ambalo hata hivyo, lilipita kwa kasi barabarani kwenda Ikulu
na kurudi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kama
ilivyokuwa imezoeleka huko nyuma, Rais wa nchi ambaye amekuwa akifika
nchini kwa mara ya kwanza, amekuwa akipita mitaani kwa gari la wazi
sambamba na mwenyeji wake akisalimiana na wananchi, hiyo imekuwa
ikifanyika pia kwa wasanii wa kigeni.
Hata hivyo,
safari hii ulinzi ulionekana kuwa mkali katika ujio wa Rais Obama na
kusababisha wenye kiu ya kumwona moja kwa moja kushindwa kufanya hivyo
isipokuwa waliokuwa na uwezo wa kufika uwanjani na katika shughuli
alizofanya maeneo kadhaa jijini.
Mapema, Rais
Kikwete alimhakikishia Rais Obama kwamba kuanzia sasa Afrika itapenda
kuona ongezeko la uwekezaji na uhusiano wa kibiashara baina yake na
Marekani.
Kikwete
alisema hayo juzi usiku katika Ikulu ya Dar es Salaam katika dhifa ya
kitaifa aliyomwandalia Rais Obama ambaye alimalizia ziara yake jana.
"Hii inaweza kuwa katika ngazi ya mataifa mawili au Taifa la Marekani na eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki,"alisema Kikwete.
Alimwambia
uzinduzi wa Mpango wa Nishati ya Umeme kwa Afrika wenye lengo la
kusaidia nchi za Kiafrika kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo ni
msaada ambao umekuja kwa wakati mwafaka.
Alisema Afrika
imekuwa ikilenga kuwa na uchumi mkubwa na hatimaye kujiletea
maendeleo, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa ni tatizo la umeme wa
kutosha.
"Hatua hii ya
Marekani kusaidia katika eneo hilo, itakwenda sambamba na kuwezesha
mataifa ya Afrika kuibua uwezo wao wa kukuza uchumi na kuboresha maisha
ya watu wao," alisisitiza Kikwete.
Alisema hatua
hiyo itaimarisha ushindani, itakuza maendeleo ya viwanda na kufanya
nchi za Afrika kushiriki vizuri katika uchumi wa dunia na kuwa wabia
katika biashara ya kimataifa badala ya kuwa wapokeaji wa misaada ya
kigeni.
"Tunakupongeza
kwa uongozi wako katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na
usalama zinazolikabili bara la Afrika. Umekuwa kishawishi kikubwa
kwetu, tunaoamini katika demokrasia, uhuru wa mtu, fursa sawa, kutokuwa
na ubaguzi na kuwa na Afrika isiyo na migogoro.
"Wewe ni
rafiki wa kweli wa Tanzania na Afrika, siku zote tutaenzi amali hizo
katika nyoyo na fikra zetu,"Kikwete alimwambia Obama.
Alieleza
matumaini ya Watanzania kwamba Obama atapata fursa nyingine ya kuja
nchini na kukaa angalau kwa muda mrefu kidogo ili ajionee mengi nchini;
nchi ambayo ina vivutio kama Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti
na Ngorongoro na kisiwa cha marashi cha Zanzibar.
Rais Kikwete
alimshukuru Rais Obama na Serikali yake na watu wa Marekani kwa msaada
wao endelevu kwa Serikali na watu wa Tanzania.
"Msaada wenu katika chakula, elimu, afya, barabara, umeme na maji umesaidia kuboresha maisha ya watu wengi nchini Tanzania.
"Naamini
uendelevu wa msaada huo utamaanisha watu wengi kuondokana na umasikini.
Kauli yako ya kutuhakikisha kwamba Serikali yako itaendelea kuisaidia
Tanzania katika maendeleo imepokewa nasi kwa mikono miwili na
unyenyekevu mkubwa," alisema Kikwete.
Akiwa Symbion,
Rais Obama aliihimiza Serikali kuhakikisha miradi ambayo itaanzishwa
chini ya mpango wa Power Africa utekelezaji wake uharakishwe ili kutoa
fursa kwa wananchi kuona manufaa yao katika kujipunguzia umasikini.
Alisema katika
mpango huo ambao Serikali yake imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni
7, alisema sekta binafsi ambayo itahusishwa kwa kiasi kikubwa katika
utekelezaji wake itatoa dola za Marekani bilioni 9.
Alisema
kutakuwa na manufaa makubwa iwapo mpango huo utahusisha Serikali na
sekta binafsi kwa upande mwingine akiongeza kuwa dhamira ya sekta
binafsi katika kutoa kiasi hicho cha fedha inaonesha nia ya Marekani
kuinua Afrika yenye nuru," alisema Rais Obama akionesha matumaini ya
mpango huo ambavyo unaweza kunufaisha nchi nyingi za Afrika.
Obama ambaye
aliitumia hotuba hiyo kuaga Watanzania, alisema Symbion ni mfano wa
miradi ambayo Marekani imedhamiria kuitekeleza Afrika ya kuongeza
maradufu uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo lengo ni kupunguza
umasikini katika bara hilo.
Alisema ili
miradi hiyo iwe na manufaa kwa nchi husika kote alikopita, alitoa mwito
kwa viongozi kuhakikisha utekelezaji unaharakishwa ili kunufaisha
nchi na kwa watu.
Alikemea tabia
ya ucheleweshaji wa miradi katika Afrika ikiwamo ya umeme lakini
akasema ana imani na uongozi wa Rais Kikwete kuwa mpango huo
utatekelezwa kwa kasi. "Ni lazima tuongoze katika utekelezaji wa miradi
hii na naamini chini ya Rais Kikwete hili linawezekana."
Alisema ili
kufanikisha kuwa na umeme wa uhakika ni vema kupunguza urasimu katika
kuhudumia wawekezaji wa sekta ya umeme ili wapate nafasi ya kuongeza
kasi ya utekelezaji wa miradi.
Aliongeza kuwa
ufanikishaji wa mpango huo utakuwa ni hatua ya ushindi kwa pande zote;
yaani kwa Tanzania ambayo itapata umeme wa uhakika ambao utasaidia
kupunguza umasikini, lakini pia kwa Marekani ambako wafanyabiashara
watapata fursa ya kuwekeza nchini.
Pia alitaka
sheria na taratibu zifuatwe na kuheshimiwa katika masuala yote ya
uwekezaji ambao utahusisha miradi itakayoanzishwa chini ya mpango wa
Power Africa.
Alipoingia ndani ya mitambo ya Symbion, Rais Obama alikabidhiwa mpira wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa gesi.
Mpira huo
ambao umebuniwa na vijana wa Kimarekani, unafaa kwa matumizi vijijini
kwani unaweza hata kuchaji vifaa vya umeme kama simu ambapo pia gesi
hiyo ina uwezo wa kuwasha taa inayoweza kutumika kumulika ndani ya
nyumba.
Rais Obama
alizindua mipira hiyo ambayo itapatikana hivi karibuni nchini kwa
kumpasia Rais Kikwete na kueleza matumaini yake kuwa inaweza kuwa na
manufaa makubwa katika maeneo ambako hayajafikiwa na umeme.
Kampuni ya
Symbion yenye makao yake makuu Washington, Marekani imeajiri Watanzania
1,000 na Rais Obama jana alitangaza kuwa ni kampuni pekee ambayo
itasimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa
na Serikali ya watu wa Marekani.
Symbion kwa
sasa inatekeleza miradi yenye uwezo wa kuzalisha umeme katika nchi za
Afrika Mashariki na Magharibi ambayo imepangwa kukamilika mwishoni mwa
mwaka huu.
Katika miaka mitano, kampuni hiyo imepanga kuwekeza kiasi cha Sh trilioni 3 katika uzalishaji umeme na njia za kuusafirisha.
Kati ya miradi
hiyo, umo wa gesi unaojengwa Mtwara wenye uwezo wa megawati 400 na
unaendeshwa kwa kushirikiana na kampuni nyingine ya Marekani ya General
Electric (GE) itakayotoa vifaa vya ujenzi katika mradi huo ambao
unahusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye umbali wa kilometa 650.
Nchini,
kampuni hiyo kwa sasa inamiliki vituo vitatu vya kuzalishia umeme wa
jumla ya megawati 217 ambavyo vipo Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.
Kituo cha Ubungo cha Symbion kinazalisha megawati 112 kwa gesi na ndiyo
kampuni inayozalisha umeme mwingi unaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mitambo hiyo
imetengenezwa mjini Houston, Texas na inaelezwa kuwa ya kisasa zaidi
yenye uwezo mkubwa wa kufua umeme kwa kasi kama ilivyo injini ya ndege.
Mitambo hiyo awali ilikuwa ya Dowans ambayo iliileta nchini baada ya
kupewa zabuni ya kufanya hivyo na Kampuni ya Richmond.
Awali baadhi
ya wabunge walishauri inunuliwe na Serikali, lakini baadhi yao
walikataa kuwa ni mitumba na sheria ya manunuzi hairuhusu. Lakini
mitambo hiyo ambayo baadhi ya Watanzania waliikejeli leo ndiyo kimbilio
la Serikali kutokana na vyanzo vya kufua umeme wa maji kupungua uwezo
wake.
Kutokana na
mapenzi mengi waliyonayo Watanzania kwa Obama, jana maelfu ya watu
walikusanyikwa Ubungo ili kumwona Rais huyo mweusi wa Marekani.
Tangu saa
mbili asubuhi Ubungo ilishafurika watu na hadi anawasili eneo hilo saa 5
asubuhi umati huo ulishaongezeka hali inayoonesha kuwa Rais huyo ni
kipenzi cha Watanzania.
Baada ya
kukagua mitambo ya Symbion, Rais Obama alisindikizwa na mwenyeji wake,
Rais Kikwete hadi uwanja wa ndege na akapanda ndege yake ya Air Force
One na kurejea Marekani.
No comments:
Post a Comment