WAZIRI wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe,
amelaumiwa na uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa kwa kushindwa
kuingilia kati mgogoro wa maji uliopo kati ya mwekezaji wa mashamba ya
mpunga Mbarali na Shule ya Sekondari ya Kilimo ya Montfort ambayo
inauziwa
maji ili kuweza kulima.
Kuibuliwa
kwa tuhuma hizo zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Waziri Maghembe
kunafuatia barua kadhaa zilizoandikwa kwenda wizarani na uongozi wa
kanisa hilo na ule wa shule hiyo pasipo kujibiwa na serikali licha ya
uwekezaji wa kanisa ulilenga zaidi kuwaendeleza vijana.
“Bado
tunaumizwa sana na suala la maji, tumeipigia sana magoti serikali ili
itusaidie tupate maji ya kutosha. Shule yetu ni ya mchepuo wa kilimo,
ilisajiliwa tukijua kuwa tutalima kwa vitendo baada ya kujiridhisha kuwa
maji yapo, tangu apewe mwekezaji ameamua kutuuzia maji,” alilalamika
Mkuu wa Shule hiyo, Ansgar Kigane.
Kigane
alisema kuwa tangu shule hiyo ilipoanzishwa miaka 25 sasa imefanya
vizuri sana kwenye masomo ya kilimo kutokana na upatikanaji wa maji
uliokuwa ukitolewa na Shirika la Kilimo na Chakula (NAFCO) kabla ya
kubinafsishwa.
“Kwa
kuwa shule yetu ni ya kilimo hasa mpunga na kwa kuwa wanafunzi waliweza
kulima na kupata mavuno ya kutosha ilikuwa rahisi kwao kupata chakula
bure shuleni, sasa hali imekuwa ngumu, mwaka huu imebidi tununue maji
kutoka kwa mwekezaji kwa masharti magumu,” alisema.
Alibainisha
kuwa licha ya jitihada kubwa za kuiomba Wizara ya Maji iingilie kati
ili kuona uwezekano wa shule hiyo kupata maji kwa kupitia mfereji mdogo
ulioruhusiwa wakati wa NAFCO, lakini wamekosa majibu sahihi.
Ofisa
Maji Mkuu wa Bonde la Rufiji ambao ndio wenye mamlaka ya kusimamia maji
katika Bonde la Usangu, Idrissa Msuya alisema kwa mujibu wa sheria ya
maji, mwekezaji aliyepewa kibali cha kuyatumia haruhusiwi kuyauza na
kwamba makubaliano yaliyofikiwa ni uamuzi wa pande mbili ambazo
haziihusu mamlaka hiyo.
Msuya
alisema kuwa mvutano huo wa maji umefumuka baada ya serikali
kubinafsisha mashamba ya NAFCO kwani huko nyuma hali haikuwa hivyo na
kwamba mamlaka hiyo imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuleta suluhu ila
anashangaa kwanini hawakubaliani.
Askofu
wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, katika barua zake
amekuwa akifanya jitihada kubwa za kuipigia magoti serikali ili iweze
kuiruhusu shule hiyo ipewe kibali cha kutumia maji kutoka kwenye mfereji
wa umma uliojengwa na serikali.
SOURCE::TANZANIA DAIMA::
No comments:
Post a Comment