SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) ambalo lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika
kuenguliwa sasa litatuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao.
Ujumbe huo ambao moja ya shughuli zake
kuwasikiliza wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF
na hawakuridhika na uamuzi huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka
huu.
Kwa mujibu wa barua ya
Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar
Tenga, kazi ya ujumbe huo ni kubaini tatizo lililopo na kutoa ripoti kwa
mamlaka zinazohusika ndani ya FIFA kwa ajili ya kutoa mwongozo.
Ujumbe huo utakutana na pande mbalimbali
zinazohusika wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini pia
ujumbe huo unatarajia kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.
Uchaguzi wa viongozi wa TFF ulikuwa
ufanyike Februari 24 mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya
baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na
wangependa shirikisho hilo liingilie kati.
No comments:
Post a Comment