Katika
gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna
habari yenye kichwa chenye maneno
‘ SIRI YA KUUAWA ZITTO YAFICHUKA’ na
vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa
atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa
kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na
wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:
Moja,
sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane
na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu
kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio
tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi
kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela
Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba
mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.
Pili,
Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua
maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi
ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa
kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu.
Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama
kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake
atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo,
fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha
niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni
kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia
ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.
Tatu,
nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie
muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya
chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA
anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa
anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina
langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la
watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa
anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye
vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda
kama ni malengo ya taasisi.
Nne,
Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu
kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk
kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu
demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama
chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache.
Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.
–
Kabwe
Zuberi Zitto, Mb
Dar-es-Salaam
Jumatano,
Machi 27, 2013
No comments:
Post a Comment