RAIS
Jakaya Kikwete ameombwa kuchukulia kwa uzito vitendo vya timuatimua
wanafunzi katika vyuo vikuu vya umma kutokana na wanafunzi hao kudai
haki wanazopaswa kuzipata wawapo vyuoni.
Msemaji
wa Umoja wa Wanafunzi waliofukuzwa katika Vyuo Vikuu nchini
(UUEST), Philipo Mwakibingwa, alitoa kauli hiyo jana wakati wa
uzinduzi wa umoja huo na kusema kuwa lengo kubwa la umoja huo ni
kutetea wanafunzi waliofukuzwa.
Alisema tangu miaka ya 2000 hadi sasa, suala hilo limezidi kukua
nchini, watawala wa vyuo vikuu ambao ni maprofesa na baadhi ya viongozi
waliopo serikalini kulichukulia kama mila na desturi.
Mwakibingwa
alisema wanafunzi hao wamekuwa wakifukuzwa kutokana na kutoa mawazo
mbadala, kuhoji mambo, kukosoa uovu uliopo na unaondelea kutendeka
ndani ya vyuo, hivyo na kutoa ushauri pale inapobidi kwa masilahi ya
taifa lao.
Akizungumzia
umoja huo, alisema wamefikia hatua ya kuunda umoja huo kutokana na
serikali pamoja na Bunge kushindwa kutatua matatizo yao na kuongeza
kuwa hali hiyo imesababishwa na taarifa potofu zilizotolewa na
watawala wa vyuo vikuu hivyo.
“Kwa
sababu watawala wa vyuo vikuu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
kututenganisha na jamii zetu, familia zetu, jamaa, viongozi wetu wa
kidini na asasi kwa taarifa za uongo kupitia vyombo vya habari, tumeona
suluhu ya maisha yetu ni kuungana. Muungano huu umeundwa kwa ajili ya
kutetea maisha yetu,” alisema Mwakibingwa.
No comments:
Post a Comment