Na Globalpublishers
VILIO
vilitawala Kata ya Nyahanga wilayani hapa wakati wa kuuaga mwili wa
binti Jessica Elialinga (19) aliyeuawa kinyama kwa kuchinjwa kama kuku
na mpenzi wake, Musa Petro (27) mkazi wa Shunu kwa sababu zinazodaiwa ni
wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo lililoibua simanzi kubwa kutokana na
marehemu kuhitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya
Nyihogo, Kahama mwaka jana, lilijiri saa 12:45 Februari 6, mwaka huu.
Kitendo
hicho kilifanyika katika banda la mbuzi lililopo nyumbani kwa kijana
huyo ambaye baada ya kutekeleza mauaji na yeye alifanya jaribio la
kutaka kujitoa roho kwa kisu.
Akisimulia juu ya tukio hilo, rafiki wa
karibu wa Musa ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa ajili ya
usalama, alisema wiki moja kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikuwa
akiwatangazia jamaa zake kwamba ana dhamira ya kumuua binti huyo
kufuatia kubaini kuwa anamsaliti kimapenzi.
“Unajua Musa anafanya
kazi ya kuchuna ngozi za wanyama machinjio ya Wilaya ya Kahama,
alitutangazia dhamira yake hiyo, lakini tulichukulia kauli yake kama
mzaha.
“Alisema anataka kufanya hivyo kwa sababu amekuwa akitumia
gharama kubwa kwa mpenzi wake huyo tangu walipoanza uhusiano, msichana
akiwa kidato cha pili, lakini anatoka kimapenzi na mwanaume mwingine,”
alisema rafiki huyo.
Hata hivyo, inadaiwa baada ya mtafaruku wa
usaliti, wawili hao walipatana na kuendelea na mapenzi, lakini baada ya
mwanafunzi huyo kuhitimu kidato cha nne alibadilika ambapo mwanaume
alisikia kuwa tayari ana mwanaume mwingine kutoka jijini Mwanza ambaye
walikubaliana kufunga pingu za maisha baada ya kumaliza masomo.
Inadaiwa
siku chache kabla ya mauaji hayo, rafiki mmoja wa karibu wa mtuhumiwa
alikutana na marehemu njiani na kumsimamisha kwa lengo la kumweleza
kauli zenye kutishia maisha yake anazozitoa mpenzi wake, lakini binti
huyo hakusimama kumsikiliza.
Baada ya Musa kudaiwa kufaulu kumchinja
mpenzi wake huyo na yeye kujikata koromeo na kuanguka akiwa ameishiwa
nguvu, kijana mchunga mbuzi ambaye wengi katika eneo hilo humchukulia
kama kaka yake Jessica, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumshuhudia Musa akiwa
katika hali hiyo.
Alipomhoji kulikoni, hakupata jibu zaidi ya
kushuhudia jitihada za mtuhumiwa huyo kufungua mlango wa chumbani mwake
zikishindikana.
Kijana huyo alitoa taarifa kwa watu ambao walifika na kumchukua Musa na kumkimbiza hospitali ya wilaya kuokoa uhai wake.
Watu
waliobaki nyumbani walifuatilia michirizi ya damu hadi kwenye zizi la
mbuzi ambako walimkuta Jessica ameshafariki dunia baada ya kuchinjwa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Everest
Mangala alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema mtuhumiwa
anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Kahama katika Hospitali ya
wilaya hiyo anakoendelea kupatiwa matibabu.
No comments:
Post a Comment