SHY - ROSE |
MBUNGE wa Afrika Mashariki Shy-Rose Bhanji
amemtaka Waziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC),
Samuel Sitta kuacha ubabaishaji kwa kutoa kauli za uongo kwa Watanzania
na badala yake aongeze kasi ya uwajibikaji.
Shy-Rose alisema hayo jana akijibu
kauli ya Waziri Sitta kwamba baadhi ya wabunge wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EALA), akiwemo yeye hawahudhurii vikao vinavyoitishwa na
wizara hiyo na kwamba wamekuwa wakidai posho.
Akijibu kauli hiyo kwa maneno makali,
Shy-Rose alimtaka Waziri Sitta na naibu wake kutoa vielelezo dhidi ya
madai yao.
“Kama nilivyosema kwenye kikao cha
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wizara
imejitenga sana katika kutoa mwongozo na vile vile katika kuwafikia
Watanzania walio wengi kwa kigezo kwamba haina fedha.
“Nimekuwa nikiwasiliana moja kwa moja
na Naibu Waziri Abdullah Juma Sadallah kuhusu masuala mengi kwa maana
ya kushirikiana na kupeana mwongozo, lakini majibu ya Naibu Waziri daima
yamekuwa ni ya ubabaishaji na ya kukatisha tamaa, akisema kwamba
wabunge wa EALA hawako chini ya wizara,” alisema Shy-Rose.
Mbunge huyo amemtaka Waziri Sitta kukaa na
viongozi wa wizara yake ili apate ukweli wa mambo kuliko kurukia kujibu
hoja kwa ubabaishaji kwani nia ni kuweka maslahi ya nchi mbele na si
binafsi kama alivyofanya juzi yeye na naibu wake kwenye kikao cha
kamati.
“Kwa vile amenitaja mimi moja kwa
moja kuwa ni kinara wa kutoa udhuru… nasema si kweli hata kidogo…
ninamheshimu Waziri Sitta kama kiongozi na kama mzazi wangu, lakini
kauli yake imenisikitisha sana sana kwani amenifedhehesha kwenye jamii
kwa kutoa kauli za kunichafulia jina langu kwa vile nimesema ukweli.
“Ni Waziri Sitta huyo huyo kwenye
kikao cha bajeti mwaka jana bungeni Dodoma nilikuwa miongoni mwa wabunge
aliowapongeza kwa kazi nzuri. Leo iweje abadili kauli yake? Au ni kwa
vile nimesema ukweli?” anahoji Shy-Rose na kuongeza kuwa penye ukweli
hatasita kuwaumbua viongozi ambao hawawajibiki.
Kuhusu suala la posho, alisema
walialikwa mara moja tu bungeni lakini waliambiwa kila mtu ajigharamie
malazi na usafiri.
“Hivi inaingia akilini kweli ualikwe
kwenda safari halafu unaambiwa ujigharamie? Yeye Sitta na Naibu Waziri
kwa vile wanatumia magari ya wizara na kuwekewa mafuta na kupewa posho
kufika bungeni ndiyo maana inamwia rahisi kuongea kiubabaishaji.
“Licha ya wizara kukataa
kutugharimia, lakini nilikuwa miongoni mwa wabunge waliohudhuria kikao
cha bajeti ya wizara huko Dodoma… hiki ni kielelezo tosha kabisa suala
la posho ni agenda ya uongo ili wizara kujisafisha kwenye kamati na
Watanzania kwa ujumla.
“Hivi inaingia akilini kweli eti
tunadai posho kuhudhuria vikao vya kupewa mwongozo tena hapa Dar?”
anahoji Shy-Rose na kuongeza kuwa suala la posho kwake binafsi
halijawahi kuwa agenda kuu hata siku moja.
“Hii hoja ya posho si ya kweli hata
kidogo, kilichoongelewa ni vipi tunafika Dodoma iwapo hatujui tutalala
wapi na tutakula nini. Sijaomba gharama hizi kama Shy-Rose bali kama
Katibu wa Wabunge wa EALA,” aliongeza.
Shy-Rose alisema ni jambo la
kusikitisha kwamba Watanzania walio wengi hawaifahamu Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa upana wake, hivyo juhudi za ziada zinahitajika kwa wizara
kushirikiana na wabunge wa EALA ili kuwafikia Watanzania wengi kufahamu
mtengamano huu.
Mbunge huyo alisema semina pekee
iliyowahi kufanyika kwa wabunge wa EALA ilikuwa mara baada ya
kuchaguliwa takriban miezi kumi iliyopita.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa na
Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na wizara, waliambiwa wizara itakuwa
inatoa mwongozo kabla ya vikao vya Bunge kuanza ili kuweka maslahi ya
taifa mbele na baada ya hapo hawajawahi kuitwa tena na wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Shy-Rose, kikao pekee
kilichoitishwa na wizara ni Januari mwaka huu jijini Bujumbura wakati
ambapo mbunge huyo alikuwa nchini India kwa matibabu.
Juzi wakati Waziri Sitta akitoa
ufafanuzi katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Sitta alisema madai ya wabunge wa
jumuiya hiyo kwamba hawashirikishwi katika vikao vya wizara yake sio ya
kweli kwani wengi ni mabingwa wa kutoa udhuru na wanataka posho.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment