OFISA Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda ametangaza kiama kwa watu wanaomiliki vituo vya kufundishia watoto masomo ya awali baada ya kubaini kuwa ndiyo chanzo cha kuwa na wanafunzi wanaongia darasa la kwanza bila kujua kusoma na kuandika.
Kaponda aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mkapa jijini hapa na kuwahusisha watendaji kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mbeya kujadili changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi.
Akitoa ufafanuzi, ofisa huyo aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa baada ya kubaini hiyo ni moja ya sababu ya kushuka kwa kiwango cha elimu mkoani hapa, ofisi yake imejipanga kuvikagua vituo vyote vya masomo ya awali.
Alisema vituo vingi vya chekechea ndiyo chimbuko la maandalizi mabovu ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza ambao licha kusoma miaka miwili, wengi wao wamekuwa hawajui kusoma na kuandika hivyo kukosa sifa ya kujiunga darasa la kwanza.
Kaponda alisema hali hiyo imechangia hata wanafunzi wanaojiunga na elimu ya kidato cha kwanza pia baadhi yao kuwa na uwezo mdogo kutokana na msingi mbovu, hivyo kushindwa kusoma na kuandika.
Aidha, ofisa elimu huyo amewatupia lawama wasimamizi wa mitihani kwa kujihusisha na rushwa na kwamba ofisi yake inaendelea kujipanga kukabiliana na changamoto hiyo.
Dk. Michaeli Kadeghe ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, alisema suala la kufeli kwa wanafunzi na baadhi yao kutojua kusoma na kuandika, ni aibu ingawa tayari taarifa zao zinaonesha kuwa wamefaulu mitihani.
Alisema mfumo wa mitaala ya elimu hapa nchini ndilo chimbuko la ubovu huu kwa kuwa haiwezekani wanafunzi wakaendelea kuwa na mfumo wa kuchagua majibu, hivyo ni mambo yanayopaswa kusitishwa haraka.
Mkuu huyo alisema kwa mfumo wa mitaala hiyo, ndiyo inawafanya hata wasiojua kusoma na kuandika kufaulu kwa staili ya kubahatisha katika mitihani yao, hivyo ni wakati mwafaka wa kufanya mabadiliko katika jambo hilo kwa wanafunzi kupimwa uelewa.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na watendaji wa serikali kutoka katika wilaya zote za mkoani hapa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na makundi mengine ya kijamii, kilikuwa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Normani Sigala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Abasi Kandoro.
Chanzo;Tanzania daima
No comments:
Post a Comment