Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za pongezi nyingi Rais Mteule wa Jamhuri ya Kenya,
Mheshimiwa Uhuru Kenyatta.
Katika
salamu hizo zilizotumwa leo, Jumamosi, Machi 9, 2013, saa chache baada
ya kuthibitishwa rasmi kuwa Mheshimiwa Kenyatta ameshinda Uchaguzi Mkuu
wa Kenya uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii Jumatatu, Machi 4, 2013, Rais
Kikwete amemwambia Mheshimiwa Uhuru Kenyatta:
“Mpendwa
Rais Mteule na Kaka, ilikuwa ni furaha kubwa kwangu kupokea taarifa ya
ushindi wako wa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya. Niruhusu, kwa
niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba
yangu binafsi kukupogenza kwa dhati ya moyo wangu kwa mafanikio haya
makubwa ya kuchaguliwa kwako.”
Ameongeza Rais Kikwete: “
Ushindi huu ni ushahidi na ishara ya wazi kabisa ya imani na matumaini
ambayo wananchi wa Kenya waliyonayo katika uongozi wako. Huu ni utambuzi
wa kazi yako maridadi na mchango wako mkubwa ambao umeutoa katika
nafasi mbali mbali za uongozi katika siku za nyuma katika jitihada zako
za kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ustawi wa nchi yako na
wananchi wake.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati
unajiandaa kuchukua madaraka ya juu zaidi katika nchi yako, napenda
kukuhakikishia msimamo wangu binafsi pamoja na ule wa Serikali yangu wa
kuunga mkono Serikali yako. Ni imani yangu kubwa kwamba pamoja tutaweza
kuendelea kusukuma mbele zaidi maendeleo ya nchi zetu – Kenya na
Tanzania na pia utengamano wa Afrika Mashariki kwa manufaa ya nchi zetu
na wananchi wake.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
9 Machi, 2013
No comments:
Post a Comment