MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda
amewataka akinamama wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali kuwa waaminifu
kwa wenza wao na wanafamilia wao ili waweze kupata ushirikiano kutoka kwao.
Alisema mbali ya majukumu mengi
yanayowakabili, akinamama wanapaswa kuwa karibu na familia zao kwani ndiyo
msingi mkuu wa Taifa. “Hatuna budi kutoa malezi mema kwa wenza wetu na watoto
wetu. Tunapofanikiwa katika shughuli zetu, tusiache kuwa waaminifu kwa wana-familia wetu (akinababa na watoto
wetu); tuwaheshimu na kuwaenzi kwa kuwashirikisha kazi tunazofanya ili tuweze
kupata ushirikiano wao na baraka zao,” alisema.
Mama Pinda ametoa kauli hiyo jana usiku
(Jumamosi, Machi 10, 2013) wakati akizungumza na wanawake wajasiriamali
walioshiriki Maonyesho Maalum ya Batik (Batik Gala Night) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani kwenye ukumbi wa Hellenic Club, Upanga jijini Dar es Salaam.
Maonyesho hayo yaliandaliwa na Kamati
ya Tamasha la Wanawake
Wajasiriamali Tanzania (MOWE) kwa kushirikiana na Ofisi ya Shirika la Kazi
Duniani hapa nchini (ILO) yalikuwa na nia ya kuamsha chachu ya kuendeleza kazi za akinamama
wanaofanya maonyesho kila mwaka yaliyopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu kwenye
Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema akinamama wanapaswa kuungana
kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kuunganisha ujuzi, stadi walizonazo
na kushirikishana uzoefu. Alisema hawana budi kuhakikisha kuwa bidhaa
wanazozalisha zinakuwa na ubora wa kiwango cha juu ili waweze kukabiliana na
ushindani kwenye soko.
“Napenda
kusisitiza, suala la ubora wa bidhaa tunazozizalisha kwa kuzingatia viwango vya
Kitaifa na kimataifa ili bidhaa zetu ziweze kupata uhakika wa soko. Hili
litafanikiwa pia endapo tutazingatia pia ubora wa vifungashio tunavyotumia
kwenye bidhaa zetu. Endapo, tutazingatia viwango, vifungashio na kutumia
kiandishi-anuani (barcodes), sioni ni kwa nini bidhaa zetu zisiende hadi masoko
ya mbali huko ughaibuni,” alisema.
Aliwataka
akinamama wajipange vizuri kwa ajili ya Maonyesho makubwa ya kitaifa (MOWE) yatakayofanyika
Oktoba mwaka huu ambayo yatajumuisha washiriki kutoka mikoa yote hapa nchini.
Mapema,
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi hapa nchini (ILO Tanzania), Bw. Alexio Musindo, alisema anawapongeza
akinamama wajasiriamali chini ya kamati ya MOWE kwani kupitia mafunzo
yanayodhaminiwa na Ofisi yake, akianamama hao wameweza kujiamini zaidi na
kuthubutu kushiriki maonyesho mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Alisema jamii haina budi kuwekeza zaidi
kwa wasichana kwa kuwapa fursa za kujiendesha kibiashara pamoja na ujuzi
(skills) ili waweze kujiajiri kwani wanakumbana na vikwazo vingi wanapotafuta
ajira ikiwemo, unyanyasaji na unyanyapaa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment