Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema
akitoa taarifa ya jeshi hilo mbele ya waandishi wa habari katika makao
makuu ya jeshi hilo leo mchana.
Nimelazimika nizungumze nanyi kuhusu
tukio la kuuwawa kwa Padre Evaristi Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar
lililotokea leo asubuhi tarehe 17 Februari, 2013 eneo la Mtoni mkoa wa
Mjini Magharibi, ambapo watu wasiofahamika walimpiga risasi Padre huyo
alipokuwa anaenda kusalisha ibada katika kanisa la Betras. Baada ya
tukio hilo kutokea alikimbizwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja, ambapo
baadae alifariki dunia. Tukio hili ni baya na la kusikitisha.
2 Kufuatia kutokea kwa tukio hilo na
kujirudiarudia kwa vitendo vya kuwashambulia na kuwadhuru viongozi wa
dini na uchomaji wa nyumba za ibada, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumeanza uchunguzi wa kina wa
kuwatafuta wanaohusika na matukio hayo.
3Hivyo, nimetuma timu ya wataalam
waliobobea kwenye masuala ya upelelezi na oparesheni kutoka Makao Makuu
ya Polisi, kwenda kushirikiana na timu ya wataalam iliyoko Zanzibar.
Hadi sasa watu watatu wananshikiliwa kwa mahojiano.
Jeshi la Polisi limeimarisha doria
maeneo yote hapa nchini na tunafuatilia mienendo na kuakamata watu wote
wanaochochea, kufadhili, kuhamasisha na kushiriki katika vitendo vya
uhalifu, vurugu na fujo.
Tukiwa katika kipindi hiki, nawaomba
wananchi wote hapa nchini kuwa watulivu wakati suala hili
linaposhughulikiwa kuhakikisha kwamba wahalifu hao wanakamatwa na sheria
inachukua mkondo wake.
Naomba nitumie fursa hii pia,
kuwasiliana na wananchi wenzangu wenye taarifa zitakazosaidia wahalifu
hao kukamatwa kutupa ushirikiano kupitia namba zetu maalum za simu
zifuatazo 0754785557 au 0782417247 na namba za makamanda wa mikoa na
vikosi, ili kuhakikisha kwamba amani, usalama na utulivu vinadumishwa
hapa nchini.
Nawashukuru wananchi wote ambao
wamekuwa wakitupa ushirikiano.
AHSANTENI SANA.
No comments:
Post a Comment