Thursday, February 21, 2013

Simanzi yatawala, Waziri azomewa


Na: Elias Msuya, Zanzibar 
SIMANZI na vilio vilitawala mazishi ya Padri Evarist Mushi yaliyofanyika Kitope Zanzibar jana huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud akipata wakati mgumu baada ya kuzomewa na waombolezaji kutokana na kukerwa na hotuba yake.Padri Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi, Jumapili iliyopita wakati akijiandaa kwenda kuongoza misa katika Kanisa la Mt. Joseph Minara Miwili mjini hapa. Ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ilianza saa nne asubuhi katika Kanisa la Mt. Joseph Minara Miwili na kuhudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Baada ya misa hiyo iliyomalizika saa 6.30 mchana, msafara wa mazishi ulielekea Kitope yalipo makaburi ya viongozi wa Kanisa Katoliki. Baada ya kufika makaburini, ibada ya mazishi ilianza saa 7.30 mchana na mwili wa Padri uliwekwa kaburini saa moja baadaye. Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa. Waziri Aboud alizomewa kutokana na kauli yake aliyotoa katika salamu za Serikali kuwa kifo cha Padri Mushi ni kazi ya Mungu, ambayo haina makosa. “Serikali imepokea msiba huu kwa
huzuni na masikitiko makubwa. Maumivu ya familia ya marehemu ni maumivu ya Serikali. Padri Mushi ametuachia pengo kubwa lakini kazi ya Mungu haina makosa,” alisema Waziri Aboud kauli ambayo ilipokewa kwa waomboleza kuguna wengine wakizomea hali iliyowafanya baadhi ya viongozi kuwatuliza.
Mmoja wa waombolezaji alisikika akisema: “Kazi ya Mungu ndiyo imewatuma hao wahalifu kuua kwa risasi?”

Mwakilishi wa familia, Francis Mushi alijibu kauli ya waziri huyo alipopewa nafasi ya kutoa salamu kwa kusema: “Tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa hasa kwa kuwa Padri hakuugua… Alikuwa kiungo kikubwa katika familia yetu.” Maneno ambayo yaliibua simanzi na vilio kutoka kwa waombolezaji wengi.

Hata Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Augustino Shao aliyekuwa amekaa karibu na Rais Dk Shein alipopewa nafasi naye alisema waziwazi: “Naomba kusema kuwa, kauli hii ya mapenzi ya Mungu haipo… Hili ni suala la uovu na tusikubali kushindwa na uovu.” Kauli hiyo ilionekana kuungwa mkono na waumini.

Ibada hiyo ilihitimishwa kwa sala iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga, Antony Banzi.
Wanasiasa waomboleza
Akizungumza baada ya kumalizika kwa msiba huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema wananchi wamechoshwa na kauli za Serikali za kuwatuliza huku watu wakiendelea kuuawa.

“Watanzania tusiendekeze kauli za Serikali za kila siku, eti Bwana ametoa Bwana ametwaa! Kifo cha Padri Mushi hakikutokana na ugonjwa wala Serikali, lakini haiwezekani kila siku Serikali iendelee na ahadi za maneno matupu.
“Haiwezekani Katibu wa Mufti, Fadhili Soraga ajeruhiwe kwa tindikali, Padri ajeruhiwe kwa risasi, kule Geita mchungaji ameuawa na mwaka jana mwandishi wa habari aliuawa na Jeshi la Polisi, tusidanganyane… tuseme ukweli,” alisema Slaa.

Akizungumzia kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kulitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na vyombo vya nje katika upelelezi, alisema: “Suluhisho siyo kuleta ‘Scotland Yard’ hapa, tatizo letu tunashughulika na matawi wakati mzizi ukiwa bado haujakatwa. Tung’oe mzizi wa tatizo.”

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alivilaumu vyombo vya usalama kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwajibika kwa mauaji yanayoendelea nchini.

“Rais anapoingia madarakani anaapa kuwa mtiifu kwa Katiba na raia wake, lakini haya matukio ya umwagaji damu yamekuwa kawaida sasa. Damu ya mtu ni ya thamani huwezi kuinunua hata uwe tajiri.”

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...