MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa watumiaji
vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini, kuwa siku zao zinahesabika
kwani ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao
itaanza kutumika na wengi huenda wakaishia gerezani.
Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kwa sasa Tanzania inaongoza kwa kuwa na
watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha
taarifa za mitandao mingi kutoaminika hadi nchi za nje kutokana na kujaa
uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa
TCRA, Innocent Mungy alikiri kuwa pamoja na kwamba mamlaka hiyo imefanya
kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo,
bado matumizi yake si mazuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na
kwa watu maarufu.
“Napenda kuwatahadharisha Watanzania na watumiaji wa mitandao hii kwa
ujumla kuwa sheria hii si ya kupuuzwa, kwani kwa hali ilivyo wengi
watatozwa faini na watashindwa kulipa na kuishia gerezani,” alisisitiza. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.