Uamuzi wa Profesa Lipumba,
mmoja wa waasisi wanne wa Ukawa-Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na
vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD-,unamaanisha
anapoteza wadhifa wake wa mwenyekiti mwenza wa umoja huo ambao umeamua
kushirikiana kwenye Uchaguzi Mkuu kwa kusimamisha mgombea mmoja kuanzia
ngazi ya urais hadi udiwani atakayeungwa mkono na vyama hivyo.
Wengine
walioongoza harakati za kuasisi Ukawa ni Freeman Mbowe, ambaye ni
mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi
wa NLD. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.
Profesa Lipumba, mmoja wa wenyeviti wanne wa
Ukawa walioeleza sababu za kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kwenye umoja huo takribani siku 10 zilizopita, jana alieleza
kuwa ameamua kujivua wadhifa huo kutokana na vyama hivyo kukubali
kupokea watu walioshiriki kukataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na
wananchi, kitu ambacho kilikuwa msingi wa kuundwa kwa Ukawa.
“Nimejitahidi
sana ndugu zangu kuvumilia, lakini dhamira inanisuta,” alisema Profesa
Lipumba mbele ya waandishi wa habari jana kwenye Hoteli ya Peacock baada
ya mkutano wa juzi aliopanga kufanyia ofisi za CUF kuzuiwa na
wanachama.
“Sisi tumekaa tunaipigia kelele Rasimu ya
Katiba ya (Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph)
Warioba lakini iliyopitishwa ni Katiba Inayopendekezwa sasa tunawachukua
waliopitisha ili waje kuisimamia. Hivi inaingia akilini?”
Lipumba aliwaomba radhi wanachama na wananchi waliomuamini wakati wote wa uongozi wake.
Tamko la maneno 900
Katika
taarifa yake ya maneno 900 ambayo aliisoma mbele ya waandishi wa habari
jana, Profesa Lipumba, ambaye amekuwa akibashiriwa kuchukua uamuzi huo
tangu katikati ya wiki hii, alisema pamoja na kujivua uongozi hatahama
CUF na kwamba ameshalipia kadi yake hadi mwaka 2020.
“Leo
hii nimeikabidhi ofisi ya Katibu Mkuu barua yangu ya kung’atuka nafasi
ya mwenyekiti wa taifa, lakini naendelea kuwa mwanachama wa CUF na kadi
yangu imelipiwa mpaka mwaka 2020,” alisema Profesa Lipumba aliyekiongoza
chama hicho kwa miaka 16.
Huku akionekana kuwa
mtulivu, alisema hajashinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote
kujiuzulu na kwamba uamuzi huo ameufanya baada ya kutafakari sana na
kushauriana na familia yake ambayo alisema imeridhia.
Mtaalamu
huyo wa masuala ya uchumi alisema ameshiriki katika vikao vingi vya
Ukawa vilivyowafikisha hapo walipo, lakini dhamira na nafsi vinamsuta
kuwa wameshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa za utu, uzalendo,
uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.
Alipoulizwa
sababu za kugeuka wakati yeye alikuwa ni miongoni mwa wenyeviti wa Ukawa
waliomkaribisha Lowassa Ukawa, alikiri akisema kuwa suala la rushwa na
ufisadi ni mfumo ambao lazima uondolewe lakini kwa sasa “dhamira yangu
na nafsi yangu vinanisuta”.
Profesa Lipumba alipotakiwa
kueleza iwapo kujiuzulu kwake kunahusiana na tuhuma za kuhongwa
mamilioni na CCM ili kuusambaratisha Ukawa, alijibu:
“Yametengwa
wapi? mimi sina taarifa hizo. Tulielezwa sisi tumemkaribisha kwa sababu
tumepatiwa mamilioni na sasa unasema mamilioni yametengwa
kusambaratisha Ukawa. Ila ninalosisitiza ni kwamba linalonipa tatizo ni
dhamira na nafsi yangu, si vingine.”
Profesa Lipumba
aliyekuwa ameongozana na mdogo wake Shaaban Miraji na rafiki yake
Abdallah Shaaban, alisema kama mwanachama wa kawaida atashiriki kampeni
za chama lakini ataendelea kuiunga mkono Rasimu ya Katiba ya Warioba.
Ukawa
iliundwa mapema mwaka jana na wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka vyama
hivyo vinne kupinga mwenendo wa chombo hicho cha kuandika Katiba,
wakisema kilipuuza maoni yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume ya Warioba na kuweka maoni yaliyotokana na
maagizo ya CCM.
Miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala
mkubwa ni muundo wa Serikali ya Muungano baada ya Rasimu ya Katiba
kupendekeza serikali tatu, na pia suala la Tunu za Taifa ambazo
zilipendekezwa kuwa ni pamoja na utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya Taifa, lakini zikaondolewa.
Kikao cha dharura CUF Zanzibar
Baadaye
jana jioni, uongozi wa CUF Zanzibar ulitoa taarifa ya kuitishwa kwa
kikao cha dharura, huku ikiwahakikishia wanachama wake kuwa itavuka
salama kwenye msukosuko huo kama ilivyofanikiwa dhoruba nyingine.
“Katika
historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi lakini
mara zote imeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili dhoruba na misukosuko hiyo
na kukabiliana na athari zake. Hatuna chembe ya wasiwasi kwamba hata
mtihani huu tutauvuka na tunaamini tutaibuka tukiwa chama imara zaidi,”
inaeleza taarifa ya CUF Zanzibar.
“Katibu Mkuu ameagiza
kuitishwa kwa vikao vya dharura vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa siku ya Jumapili, tarehe 9 Agosti, 2015
ili kujadili hatua hiyo na kufanya uamuzi juu ya hatua muafaka
zinazopaswa kuchukuliwa katika kipindi hiki hadi hapo chama
kitakapomchagua mwanachama mwingine kujaza nafasi hiyo ya mwenyekiti.”
Kuondoka
kwa Lipumba kunaacha nafasi mbili za juu kuwa wazi baada ya aliyekuwa
makamu mwenyekiti, Juma Duni Haji kuhamia Chadema na kupitishwa kuwa
mgombea mwenza wa Ukawa kutokana na makubaliano ya kimkakati ya vyama
vinavyounda umoja huo. Hali hiyo inafanya kiongozi mkuu kwa sasa kuwa
Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
CUF wajibu mapigo Dar
Nusu
saa baada ya kutangaza kujivua uenyekiti, uongozi wa CUF jijini Dar es
Salaam uliitisha mkutano wa ghafla na wanahabari kwenye ofisi za makao
makuu yake zilizoko Buguruni na kueleza kuwa kama kiongozi, Profesa
Lipumba ana uhuru na haki kikatiba kujiuzulu na CUF kama taasisi bado
ipo imara. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.
“Tunakubaliana na uamuzi wake, lakini
tuwaeleze wanachama wetu na Watanzania kwa ujumla kuwa uongozi wa CUF
umebaki imara na unaendelea na shughuli zake kwa kufuata taratibu zote
na vikao vyetu vitaendelea kama kawaida. Bado katibu mkuu yupo na
viongozi wengine wapo,” alisema mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF,
Mustafa Wandwi.
Aliwatoa hofu makada wanaogombea ubunge
na udiwani akiwataka waendelee na mikakati yao ya uchaguzi kwa sababu
uamuzi wa kugombea umebarikiwa na Baraza Kuu la Uongozi na hakuna
mfarakano wowote ndani ya chama.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Profesa Lipumba kuwa Ukawa imevunja misingi na maadili wanayoiamini, alisema:
“Yeye
alikuwa kiongozi wetu mkuu na aliridhia mengi kama kiongozi wa chama na
yapo maandishi yanayoonyesha tulivyoridhia ndani ya Ukawa na
tunaendelea vizuri bila tatizo lolote katika umoja huo.
“Kama
amegundua udhaifu huo sasa, anaujua yeye kama kiongozi na mwanachama.
Sisi hajatupatia taarifa rasmi katika kikao cha aina yoyote na siwezi
kuyazungumzia kwa sababu kama chama hatujajadili hayo na tukijadili
tutatoa maelezo.”
CUF bila Lipumba
Wakati
uongozi ukieleza hayo, makada waliokuwa makao makuu ya CUF walikuwa
katika makundi wakijadili kung’atuka kwa Profesa Lipumba huku wengi
wakisema “CUF bila Lipumba inawezekana”.
Ili kuondoa
simanzi na taharuki, walianza kushawishiana kuimba nyimbo za hamasa
zikiwamo za “tuna imani na Ukawa, hoyaa, hoyaaa…tuna imani na Lowassa
hoyaa, hoyaaa” na kuchagiza pia salamu ya maarufu ya CUF ya “CCM kwisha
kwisha kwisha kabisa, mlalo wa chali, kifo cha mende, kwisha kabisa”.
“Taarifa
za kujiuzulu imetushtua sana, mheshimiwa hakutumia hekima na busara,”
alisema katibu wa vijana Kata ya Magomeni, Salim Mzee. Jana (juzi) wazee
na viongozi wa dini walimwita kujadiliana lakini inaonekana alikuwa na
chuki katika nafsi yake na kama kulikuwa na tatizo ndani ya Ukawa
angetuita tukajadiliana lakini kama wana-CUF hatutatoka ndani ya Ukawa
na tutajenga chama kuhakisha tunaing’oa CCM,” aliongeza.
Licha
ya Profesa Lipumba kueleza kuondoka kwake hakuhusiani na kupatiwa
mamilioni ya fedha kuvuruga Ukawa, kada Abdallah Mohamed alisema
kuondoka kwa Lipumba siyo bure kuna mkono wa CCM.
“Juzi
tu alikuwa akitoa kauli za wazi mbele ya vyombo vya habari kuhusu
kuunganisha nguvu ya Lowassa na Ukawa CCM chali, chali, mlalo wa mende,
sasa kwa hapa nani kawa mlalo wa mende?
Chadema walonga
Mwanasheria
mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hatua ya Profesa Lipumba kujiuzulu
ni sawa na jenerali wa jeshi aliyeanguka katikati ya mapambano ya
kuelekea Ikulu na harakati za mageuzi na mabadiliko alizoanza miaka 20
iliyopita.
Akizungumza nje ya Hoteli ya Ledger Bahari
Beach kilipofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana, Lissu alisema
katika mapambano kuna majenarali na askari wa kawaida, lakini Profesa
Lipumba ni sawa na jenerali aliyeanguka katikati ya uwanja wa mapambano
ya mabadiliko.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la
chama hicho (Bawacha), Halima Mdee alisema Profesa Lipumba alikuwa
kikwazo katika maamuzi ya Ukawa.
“Sishangai kwa sababu
tulikuwa tunajua kuwa yeye ndiyo kikwazo cha Ukawa tangu mwanzo wa vikao
vyetu. Alikuwa na sababu nyingi, akimaliza hii anaibua nyingine,”
alisema Mdee.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa alimfananisha Profesa Lipumba na abiria wa treni anayeamua
kushukia njiani kabla hajafika anakokwenda. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment