MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na vyama vingine
vitatu vya upinzani vinavyounda umoja unaofahamika kwa jina la Ukawa,
Edward Lowassa jana alichukua fomu za kuwania rasmi nafasi hiyo kutoka
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani aliyejiunga Chadema hivi karibuni
baada ya kushindwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi
ya CCM, sasa ameungana na wagombea wengine kujitokeza NEC kuchukua fomu
za kuwania urais.
Ametanguliwa na mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ambaye pia ni Waziri
wa Ujenzi na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa. Wengine ni Mchungaji
Christopher Mtikila wa DP, Mac-Millan Lyimo wa TLP, Hashim Rungwe wa
CHAUMMA, Chifu Lutasola Yemba wa ADC na Dk Godfrey Malisa wa CCK. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.
Lowassa alianza msafara wake saa tano asubuhi akitokea ofisi za Chama
cha Wananchi (CUF), Buguruni alikuwa kwenye msafara mrefu huku
akisindikizwa na mamia ya wafuasi wa vyama hivyo na kupita barabara ya
Uhuru, na baadaye Bibi Titi na kuja hadi Ohio.
Akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba T 878 CFU
alifika ofisi za NEC zilizopo makutano ya mitaa ya Ghana na Ohio,
katikati ya Jiji la Dar es Salaam, majira ya saa 7:30 mchana akiambatana
na mgombea mwenza Juma Duni Haji, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi James Mbatia, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Pia walikuwapo baadhi ya wabunge wa vyama vya Chadema, Cuf na
NCCR-Mageuzi na viongozi wa juu wa vyama hivyo. Baada ya kuchukua fomu
na kuonesha wananchi, Lowassa alianza safari ya kuelekea Kinondoni
kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema kwa gari huku akisindikizwa na
maelfu ya wafuasi vya vyama hivyo waliokuwa wanatembea kwa miguu kutoka
ofisi za NEC.
Kutokana na umati wa watu uliofurika katika ofisi za Chadema, Lowassa
na msafara wake walilazimika kutumia uwanja wa Biafra kwa ajili ya
kuwaaga wafuasi waliotembea kwa miguu kumsindikiza.
Akizungumza akiwa kwenye ofisi za Chadema, Lowassa mbali na
kuwashukuru wafuasi wao kwa kujitokeza alisema agenda yake ya kwanza
akiingia Ikulu ni kuondoa umasikini kwa makundi yote.
Alisema asilimia 72 ya wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu, ni
vijana hivyo anawaahidi kushughulikia matatizo yao kupitia ilani ya
Chadema ambayo inatarajia kutolewa muda si mrefu.
“Nikiingia Ikulu nachukua dhamana ya kushughulikia matatizo ya
vijana, nitaunda serikali ambayo ni rafiki kwa mama ntilie na waendesha
bodaboda. Tutakuza uchumi kwa kasi kubwa,” alisema. Asante kwa kutembelea blog hii, endelea kuwa nasi, like page yetu ya facebook bofya neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment