Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Watu wanne wamejeruhiwa
baada ya milipuko minne inayoaminika kuwa ni mabomu kutokea katika
maeneo matatu tofauti Zanzibar.
Katika moja ya matukio hayo, watu
wanne walijeruhiwa, mmoja akikatika mguu, katika eneo la Unguja Ukuu,
Mkoa wa Kaskazini Unguja. Majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya
Mnazi Mmoja, Unguja.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Mkoa wa
Kusini Unguja, Hamad Said Masoud alisema mlipuko wa kwanza ulitokea juzi
katika eneo la Fuaoni Maili Nne wakati watu wasiojulikana waliporusha
kitu kinachoaminika kuwa ni bomu wakati waumini wa Kanisa la Evangelist
wakiendelea na ibada ya Jumapili.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan
Omar Makame alisema tukio la juzi, kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu
kilirushwa wakati waumini wa kanisa hilo wakiendelea na ibada na kutoa
mlipuko na kishindo kikubwa. Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi wa
tukio hilo, milipuko mingine mitatu ilitokea jana.
Katika mlipuko wa kwanza kwa jana
uliotokea saa 6.30 mchana katika kituo kimoja cha fundi vyuma
aliyetambulika kwa jina la Juma Abdallah huko Unguja Ukuu ndiko
kulikokuwa na watu waliojeruhiwa.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Pandu Haji Pandu aliyekatika mguu na Shaaban Khamis Ibrahim ambaye aliumia sehemu za kiuno.
Hamad alisema mtu mmoja aliokota chuma kizito na kukipeleka kwa fundi akitaka atengenezewe nanga kwa ajili ya uvuvi.
Alisema mhunzi huyo alipokea kazi hiyo
na alipokuwa akijiandaa kwa matengenezo ndipo mlipuko huo ulipotokea.
Mlipuko huo ulitokea sambamba na mwingine katika Mgahawa wa Mercury's
uliopo Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi na kusababisha huduma za chakula
kusitishwa kwa muda.
Tukio la mwisho lilikuwa saa 7:15
mchana katika Kanisa la Anglikana, Mkunazini. Katibu wa Kanisa hilo
Dayosisi ya Zanzibar, Nuhu Saranya alisema: "Nilisikia kishindo cha
mlipuko, wakati nikitafakari ni kitu gani hicho, nikasikia mlipuko wa
pili nje ya kanisa letu," alisema.
Mmoja wa majeruhi, Mohamed Ibrahim
alisema hakujua kilichotokea huku akilalamika kuwa masikio yake
hayasikii vizuri kutokana na kishindo hicho.
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-like page ya facebook ya Jambo Tz