UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa
unaovuma kuelekea kambi ya upinzani, sasa unaonekana kuwaamsha viongozi
wa vyama hivyo baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa wanafikiria
kusimamisha mgombea mmoja wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
kabla ya kuthibitishwa na mmoja wa viongozi hao, zilieleza kuwa hatua ya
vyama hivyo imekuja baada ya ushirika wao waliouunda kupinga upungufu
uliokuwemo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kuzaa matunda.
Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa maamuzi
hayo magumu ya wapinzani yametiwa chachu na kauli aliyoitoa Rais Jakaya
Kikwete ya hivi karibuni ya kukitabiria anguko Chama Cha Mapinduzi
(CCM), katika uchaguzi wa mwaka 2015 au ule wa 2020, kutokana na kile
alichodai kuwa viongozi wa chama hicho kuendekeza rushwa.
Mmoja wa viongozi wanaounda ushirika
huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alithibitisha taarifa hizo huku akisisitiza kuwa nia ya kufanya hivyo ni
kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mbatia, walichokifanya
kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si nguvu
ya soda na badala yake wataendeleza hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.