Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa
Kulinda Amani, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (Monusco),
Luteni Rajab Ahmed Mlima, alikuwa katika hatua za mwisho za kufunga
ndoa.
Askari huyo aliuawa katika uwanja wa mapambano na
vikosi vya wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23, katika Milima ya
Gavana, karibu na Goma, DRC- Congo wakati akitekeleza jukumu la ulinzi
wa amani
Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk
Aziz Mlima, alisema kuwa ndugu yake alikuwa tayari amekamilisha mipango
yote na kilichokuwa kikisubiriwa ni siku ya kufunga ndoa hiyo.
“ Alikuwa yuko mbioni kufunga ndoa, lakini kwa
sasa sitapenda kutaja jina la mchumba wake kwa kuwahayupo hapa lakini
naye ni askari,” alisema Dk Mlima.
Alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili
nchini leo ukitokea Entebbe, nchini Uganda, ulikopelekwa kwa ajili ya
uchunguzi wa kitabibu.
JWTZ yatoa tamko
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya
JWTZ, ilisema askari huyo alipigwa risasi wakati akiwalinda wananchi
wasidhurike na mapigano kati ya Jeshi la Serikali ya DRC na wapiganaji
wa Kundi la M23.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema Monusco inajipanga
kuuleta mwili wa marehemu na wananchi watajulishwa taratibu za mapokezi,
kuaga mwili na mazishi.
Ofisa huyo anakuwa wa pili wa JWTZ kuuawa katika
mapigano nchini humo, baada ya hivi karibuni Meja Khatib Shaaban
Mshindo, kuuawa kwa bomu katika mapigano makali yaliyotokea katika mji
wa Goma, Agosti 28, mwaka huu.
Julai 13, askari saba wa Tanzania waliokuwa
wakilinda amani katika mji wa Darfur nchini Sudan, waliokuwa katika
mpango wa kulinda amani, waliuawa na kikundi cha Janjaweed.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment