Rais wa jamuhuri ya muungao wa Tanzania Dr. John Magufuli, leo
anatarajia kuzindua ukuta wa machimbo ya madini ya Tanzanite, iliopo
eneo la Mererani, mkoani Arusha.
Ukuta huo wenye
urefu wa kilomita 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu, umejengwa
kufuatia agizo lililotolewa na Rais John Magufuli, kama jitihada za
kudhibiti na kuzuia utoroshwaji wa madini hayo, ambayo yanapatikana
nchini Tanzania pekee.
Mwezi Februari mwaka huu, wakuu wa vyombo vya usalama, walitembelea eneo
hilo, kuukagua ukuta huo uliojengwa kwa gharama za Kitanzania isiyozidi
bilioni 6.
Walisisitiza kuwa lengo la kujengwa kwake ni kuzuia uhalifu na si kuwazuia wachimbaji wakubwa na wadogo kupata riziki zao.
Wakitoa taarifa kwa viongozi wa ulinzi, wataalamu waliojenga ukuta
huo, walisema licha ya kufanikisha ujenzi huo, changamoto mbalimbali
walikutana nazo ikiwemo hatari inayoukabili ukuta huo, kutokana na
wachimbaji kulipua baruti, karibu na ukuta, hivyo kusababisha hatari za
kuharibika haraka. Ugumu wengine walioupata ni uchimbaji katika maeneo yenye miamba.